Vikapu Bomba yapata rukuzu kuchochea uzalishaji vikapu

KAMPUNI ya Vikapu Bomba inayofanya kazi na wanawake wa vijijini zaidi ya 300 mkoani Iringa na mikoa jirani imepata ruzuku ya Sh Milioni 243 kutoka Taasisi ya Marekeni ya Maendeleo Afrika (USADF) itakayotumika kuchochea uzalishaji wa vikapu kwa matumizi ya soko la ndani na nje.

Mbali na kuchochea uzalishaji kwa kutoa mafunzo yatakayowawezesha wanawake hao kutengeneza vikapu bora zaidi, sehemu ya ruzuku hiyo itatumika kama mtaji wa Vikapu Bomba kwa ajili ya ununuzi wa vikapu vingi zaidi, kuboresha miundombinu yao ya kulifikia soko la ndani na nje kirahisi na kugharamia shughuli mbalimbali za uendeshaji wa ofisi.

Kampuni hiyo inayofanya kazi na kuwasaidia wanawake hao imepata ruzuku hiyo baada ya andiko lake la kuendeleza na kuinua sekta hiyo inayokuza ajira kwa wanawake, kushinda katika mchuano ulioshirikisha waombaji zaidi ya 250 nchini.

Akizungumza katika halfa ya utoaji wa rukuzu iliyofanyika Gangilonga, mjini Iringa, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Peres Magiri alisema; “Fedha hizo zitasaidia kutengeneza zaidi fursa za ajira kwa wanawake wa wilaya yake na maeneo mengine wanaojishughulisha na biashara hiyo.”

“Naipongeza Vikapu Bomba kwa namna inavyoisaidia serikali kutengeneza ajira mpya, wanawake wanaofanya kazi na kampuni hiyo hawatapata tu mapato thabiti, bali pia wataweza kujisaidia wenyewe na familia zao kupitia biashara hiyo,” alisema.

Mratibu wa Programu za USADF nchini, Gilliard Nkini, alisema fedha iliyotolewa kwa Vikapu Bomba ni sehemu ya ruzuku wanazotoa kupitia moja ya programu zao inayojulikana kama Academy for Women Entrepreneurs (AWE) ili kuwawezesha wanawake kufikia ndoto zao katika ujasirimali na kubadili maisha.

“Miongoni mwa mambo tuliyozingatia kabla ya kuichagua Vikapu Bomba kuwa moja kati ya mashirika yaliyopata ruzuku hiyo ni pamoja na kujiridhisha shirika linamilikiwa na waafrika wenyewe na lililoonesha matokeo ya moja kwa moja kwa jamii za vijijini inazofanya kazi,” alisema.

Kwa upande wake, Mratibu wa Shirika la ADC Tanzania linaloisaidia USADF kuratibu matumizi ya fedha hizo, Eileen Mwakisese, alisema kwa kupitia ruzuku hiyo wana matarajio makubwa kuona mapato na ustawi wa wanawake hao unaongezeka.

“Nawapongeza Vikapu Bomba kwa kupata ruzuku hii.

Hii ni mara ya pili kwao kupata ruzuku kutoka USADF kwa lengo la kufanya kazi na kuwasaidia wanawake hususani wa vijijini, mara ya kwanza walipata Dola 10,000 na mafanikio yao yamewapandisha hadi Dola 100,000. Kwa kweli wanahitaji pongezi,” alisema.

Alisema kwa kuongeza kipato cha mwanamke, inatarajiwa ubora wa maisha yao utaongezeka na watakuwa na uwezo wa kusaidia familia zao wakiwemo watoto kwenda shule.

“Tunaona maendeleo na ubora wa bidhaa zinazotengenezwa na Vikapu Bomba kwa sababu hiyo itawasaidia kuvamia masoko yasiyofikiwa ulimwenguni,” alifafanua.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Vikapu Bomba, Catherine Shembilu aliishukuru USADF kwa ruzuku hiyo akisema inakwenda kutatua changamoto kadhaa zilizokuwa zinazuia ukuaji wa Vikapu Bomba kwa muda.

“Nilifurahi sana nilipoambiwa kuwa Vikapu Bomba ilishinda ruzuku hii kwa sababu niliwaza mara moja jinsi itakavyobadilisha maisha ya wafumaji vikapu na shirika letu kwa ujumla,” alisema.

Shembilu alisema kwa kadri anavyofanya kazi, ndivyo anavyojifunza kwamba wanawake wengi wanapenda kupata fursa ya kushirikiana na Vikapu Bomba kukuza ujuzi wao na kutanua soko la bidhaa za vikapu wanavyozalisha.

Kwa ruzuku hii, tutaweza kuwakaribisha wanawake zaidi nchini Tanzania na kuwafundisha wafumaji tunavyofanya kazi nao ili kukidhi viwango vya ubora vya kimataifa.

Safari ya Shembilu katika biashara yake hiyo ya vikapu ilianza mwaka 2011 akifanya kazi na wanawake sita ambao sasa wameongezeka hadi zaidi ya 300.

“Katika safari yetu ya kujenga kampuni, niligundua kwamba wanawake hawa walikuwa wakiuza vikapu vyao vizuri sana kwa bei nafuu ambayo ilikuwa vigumu kuwawezesha kuendelea. Iliniuma moyo kuona kiasi kikubwa cha kazi ngumu kikipuuzwa. Nilihisi kuwa na azimio la kuhakikisha wanapata faida sawa kwa juhudi zao ndipo tukaanzisha Vikapu Bomba, inayoeleweka kama Vikapu Vizuri,” alisema.

Alisema mbali na soko la ndani Vikapu Bomba vinauzwa katika nchi zaidi ya 20 duniani, ikiwa ni pamoja na Marekani, Uingereza, Canada, Finland, Afrika Kusini, Australia, na Denmark.

Wanawake wengi wa wilaya ya Kilolo wanaofanya kazi na Vikapu Bomba wameshukuru ushirikiano wao na Vikapu Bomba wakisema umewawezesha kuongeza mapato yao kwa wiki ambayo ni kati ya Sh 60,000 na sh 150,000.

Mmoja wa wanawake hao, Fanula Nyamoga mama wa watoto watano alisema; “Nimeanza Vikapu Bomba mwaka 2016, familia na mume wangu wananiheshimu kwasababu kipato change kimeongezeka, nasomesha watoto na gharama zamahitaji mengi.”

Mmojawa wateja wa Vikapu Bomba, Irine Kaiza amezungumzia ubora wa Vikapu Bomba akisema vinajulikana kwa ubora wake na thamani kwa wateja kwani vinatengenezwa kwa ufundi wa hali ya juu, malighafi bora, vina muundo wa kipekee na ubunifu wa kisanii.

Habari Zifananazo

Back to top button