Vikosi kazi zaidi kuundwa

RAIS Samia Suluhu Hassan amepokea ripoti ya Kikosi Kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi yenye mapendekezo mbalimbali ambayo amesema ataunda vikosi kazi ndani ya serikali kuyafanyia kazi.

Alisifu kazi nzuri iliyofanywa na kikosi hicho akisema baadhi ya mapendekezo ni mepesi na yanaweza kufanyiwa kazi haraka lakini mengine yatalazimu kukaa na kuangalia sheria zilizopo kujua upungufu uliomo na namna ya kubadilisha kulingana na mapendekezo hayo.

Kikosi kazi hicho kilichoundwa Desemba 23, 2021 kikiwa na wajumbe 24 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake, Profesa Rwekaza Mukandala, kiliwasilisha ripoti hiyo kwa Rais Samia jana Ikulu, Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kupokea ripoti ya kikosi kazi hicho kilichozinduliwa Januari 11 mwaka huu, Samia alisema vikosi kazi atakavyounda ndani ya serikali vitajumuisha watunga sheria, wataalamu wa masuala ya siasa, katiba na wataalamu wafanyie kazi mapendekezo ya ripoti hiyo.

“Kwa hiyo siyo jambo ambalo leo tumekabidhiwa na kesho tunaanza kutekeleza maoni ya kikosi kazi, hapana. Lakini kikosi kazi kimetupa mambo mazuri ya kuyazingatia na kuyafanyia kazi serikalini. Kwa ufupi niseme tumepokea na tutayafanyia kazi,” alisema.

Alisisitiza: “Na nikisema hivyo, wananchi nao wanisikie kwamba tumeyapokea na tutayafanyia kazi.”

Alisema wananchi wanapaswa kujua kuwa maoni hayo ya kikosi kazi si mwisho wala amri kwa serikali kwamba lazima iyatekeleze, bali watayatekeleza kwa kuangalia hali halisi ndani ya serikali na sheria nyingine zilizopo.

Miongoni mwa mapendekezo aliyozungumzia ni juu ya marekebisho ya sheria ndani ya vyama vya siasa kuona kama inakidhi matakwa ya usawa wa kijinsia, matumizi mazuri ya fedha, masuala ya utawala bora badala ya kuvigeuza vyama hivyo kuwa binafsi.

“Katika kikosi kazi, wengi ni wa vyama vya siasa, lakini mmeweza kujichambua na kusema tuangaliwe na sisi tunakwendaje, kwa hiyo ni kazi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi na watu wake,” alisema.

Aliendelea: “Tutawawezesha na wenyewe waweze kufanya hivyo, kujitathmini wenyewe. Ni jambo zuri, lakini lazima kuwe na mwingine anayewatazama mnavyojitathmini.”

Rais alikubaliana na asilimia 40 iliyopendekezwa na kikosi kazi kuhusu mambo ya jinsia ndani ya vyama vya siasa, hususani kuanzia katika chama chake ambako alisema wanajitahidi kufanya vizuri, jambo alilosisitiza vyama vingine kufanya hivyo.

Kuhusu pendekezo la ruzuku kwa vyama vya siasa, alisema mambo yaliyopendekezwa ni mengi na ambayo yanaleta athari ya gharama kwa serikali.

“Tutatoa ruzuku lakini mgawo ukoje? Itategemea kama kugawana kwa misingi hii ambayo imeletwa na kikosi kazi, itabidi mfuko uleule ugeuzwe kwenye mpango huu ambao mmeusema. Hatuwezi kuongeza fedha zaidi kwa sababu ni masuala ya bajeti na bajeti kwa mwaka huu ilishapita,” alisema Rais Samia.

Mapendekezo mengine ambayo alisema serikali itayafanyia kazi ni bajeti ya Msajili wa Vyama vya Siasa, muundo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na matumizi ya teknolojia kwenye tume hiyo, mijadala ya kitaifa ya kisiasa kila mwaka, ukatili wa kijinsia katika vyama vya siasa na rushwa katika vyama wakati wa uchaguzi.

 

Habari Zifananazo

Back to top button