Vikundi vipya 17,330 vyasajiliwa TPLMIS mikopo ya 10%

SERIKALI imesema jumla ya vikundi vipya 17,330 vimesajiliwa tangu kuanza kwa mfumo mpya wa mikopo ya halmashauri unaotumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TPLMIS) kwa ajili ya kutoa asilimia 10 ya fedha za ndani kwa vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu.

Kati ya vikundi hivyo, 1,207 vimepatiwa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 9.5 kwa mwaka wa fedha 2022/23. Akizungumza na HabariLEO jana, Mkurugenzi wa Idara ya Serikali za Mitaa kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk Angelista Kihaga alisema mfumo huo TPLMIS, ulianzishwa kwa lengo la kuondoa changamoto zilizokuwepo awali zikiwamo vikundi kujisajili zaidi ya mara mbili.

Pia vikundi kutorejesha mikopo kwa wakati na uwasilishaji wa maombi kwa njia ya mikono. “Vikundi hujisajili kwa kutumia mfumo huu wa https:mikopohalmashauri.tamisemi. go.tz/login kwa kutumia simu janja na kompyuta na maofisa Maendeleo ya Jamii wapo katika tarafa zote kwa ajili ya uwezeshaji wa usajili na maombi ya mikopo kwa kutumia mfumo huu,” alisema. Dk Kihaga alisema mafanikio ya mfumo huo yametokana na Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma Awamu ya Pili (PS3+) unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID).

Alisema ushirikiano baina ya mradi huo na mamlaka za serikali za mitaa kwa pamoja wameweza kufanya kazi na watendaji kata, vijiji na mitaa kuwahamasisha wanawake, vijana na wenye ulemavu kuhusu uwepo wa mikopo ya asilimia 10, namna wanavyoweza kupata mikopo na kurejesha mikopo ili kuweza kubadilisha maisha yao.

Alieleza kuwa katika mwaka wa fedha 2022/23 jumla ya Sh bilioni 76.02 zimetengwa kwa ajili ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kati ya fedha hizo Sh 30,408,071,006 ni kwa ajili ya vikundi vya wanawake, Sh 30,408,071,006 kwa ajili ya vikundi vya vijana na Sh 15,204,035,503 kwa ajili ya vikundi vya watu wenye ulemavu.

Pia alisema kupitia mfumo huo vikundi vina uwezo wa kujua hali ya marejesho ya mikopo yao kwani kuna moduli ya ufuatiliaji inayomuwezesha ofisa maendeleo ya jamii kupata taarifa za kikundi kwa urahisi kwa sababu mfumo huo una taarifa za vikundi na idadi ya vikundi vinapopatikana nchini.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
TPLMIS
TPLMIS
2 months ago

TPLMIS

Back to top button
1
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x