OFISI ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa imeanza kutoa mafunzo maalumu ya kuvijengea na kuimarisha ujuzi wa uokoaji vikundi vya uokoaji vya wavuvi mkoani Kagera.
Hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya serikali baada ya ajali ya ndege ya Kampuni ya Precision iliyotokea Novemba 6, 2022 na kusababisha ndege hiyo kuanguka katika Ziwa Victoria na kuua abiria 19 na wengine 24 kunusurika.
Mafunzo hayo yanayofanyika kwa wavuvi wa wilaya za Bukoba, Misenyi na Muleba mkoani humo yanalenga kuwaongezea wavuvi mbinu na utayari wakati wanafanya uokoaji endapo inatokea ajali iwe ya majini, nchi kavu au angani.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Selestine Masalamado alisema mafunzo hayo yanalenga kupunguza athari zinazojitokeza zinapotokea ajali au majanga.
Masalamado alifafanua kuwa utaratibu wa kuwajengea uwezo vikundi vya wavuvi utaendelea katika maeneo mengine ya maziwa makuu na bahari ili kuhakikisha wanapata mbinu za kisasa katika uokoaji.
“Ajali inapotokea kila mmoja anakuwa na mawazo binafsi kuhusu hatua za kuchukua ili kuokoa maisha ya watu na mali na matokeo yake ni kulinda na kukuza uchumi. Ikumbukwe wakati wa kuokoa watu katika ajali au majanga hata mwokoaji anaweza kupoteza maisha, hivyo ajali ya Precision imetupatia somo la umuhimu wa kutoa mafunzo kwa vikundi hivi vya wavuvi,” alisema.
Mafunzo hayo yanatolewa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Polisi upande wa wanamaji, DARMART.
Pamoja na mafunzo hayo, Ofisi ya Waziri Mkuu imewawezesha wavuvi kwa kuwapa vifaa maalumu vinavyotumika wakati wa uokoaji ili wavitumie wakati wa shughuli zao za kawaida za uvuvi na endapo ajali itatokea waweze kuvitumia kufanya uokoaji.
Awali akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila aliwataka walengwa kutumia mafunzo hayo kama fursa ya kujiendeleza katika sekta mbalimbali huku akiwataka baadhi ya watu wanaozungumzia matokeo ya ajali ya ndege ya Kampuni ya Precision kuwa na mtazamo chanya kuhusu hatua na taarifa inayotolewa kwa umma kwa sababu taarifa zinazotolewa inakuwa ni baada ya uchunguzi.
Mvuvi Rachard Mulashani alisema: “Jambo hili halijawahi kutokea. Sisi wavuvi jamii inatuona kama watu wa hali ya chini, lakini serikali imetambua mchango wetu katika uchumi wa nchi na kuamua kutuletea mafunzo hadi kwetu.”
Akizungumza wakati wa kuaga miili ya watu 19 waliokufa kutokana na ajali hiyo Novemba 7, mwaka huu katika Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliagiza zifanyike hatua za kutambua mchango wa vikundi vya wavuvi walioshiriki katika uokoaji kwa kuwapatia mafunzo, nyenzo na vifaa kwa ajili ya kuimarisha ujuzi na utayari wakati wa maafa.
Novemba 9, mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan alitoa Sh milioni kumi kwa vikundi vya wavuvi walioshiriki wakati wa uokoaji wa waathirika katika ajali hiyo ikiwa ni utambuzi wa jitihada na mchango wao katika uokoaji wa maisha ya watu na mali.