Vinara wanaochafua mazingira kukamatwa

OFISA Mazingira wa Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro amewaagiza watendaji wote wa kata 41 na mitaa zaidi ya 220 kuwakamata vinara wanaochafua mazingira ya mifereji ya maji machafu kwa kutupa takataka.

Agizo hilo lilitolewa wakati alipokuwa akizungumza na wakazi wa kata za Miyuji na Mnadani Jiji la Dodoma baada ya kumalizika usafi wa mazingira.

Kimaro aliwataka watendaji wa kata na mitaa kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao kwa kuwakamata wanaochafua na kuharibu mazingira ya mifereji ya maji taka.

Advertisement

Alisema usafi unatakiwa kuwa sehemu ya tabia ya mtu hivyo uanzie nyumbani kwa kufanya usafi na kutunza mazingira na watendaji wote wa kata, mitaa na mabalozi wahakikishe wanasimamia.

Alitaka wasiofanya usafi na kuchafua mazingira kwa makusudi wasionewe aibu bali wakamatwe na kupewa adhabu kwa mujibu wa sheria bila kuoneana huruma.

Pia aliwataka wananchi kujenga tabia ya utamaduni wa kufanya usafi wa mara kwa mara kwenye maeneo yao ili kuipa hadhi Jiji la Dodoma ambalo ni makao makuu ya nchi.

Alisema licha ya Dodoma kuwa makao makuu lakini bado kuna changamoto kwa baadhi wa wakazi wanaoendelea kuchafua mazingira pamoja na elimu inayotolewa.

“Ufanyaji wa usafi wa uhakika unapunguza magonjwa kwa asilimia 75, yakiwemo ya milipuko kama vile kipindupindu ambayo huigharimu serikali mabilioni ya fedha pindi magonjwa hayo yanapojitokeza.”

“Lazima tutambue kuwa usafi ni sehemu ya kupunguza magonjwa kwa asilimia 75 yakiwemo ya milipuko kama vile kipindupindu ambao hugharimu mabilioni ya fedha kwa ajili ya kutibu ugonjwa huo jambo ambalo pia ni fedheha kwa magonjwa yatokanayo na uchafu,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Karume, Kata ya Mnadani, Matwiga Kyatya amehimiza wananchi wa kata hiyo kuhakikisha wanaimarisha ulinzi na usalama kwenye maeneo yao na kuwataja bila kuwaonea aibu na wanaojihusisha na wanaonekana kuwa tishio wa amani na usalama katika kata hiyo.

Mwenyekiti Kata alisema ili kulinda usalama wa maeneo husika ni lazima kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake na inapotokea vitendo vya uharibifu taarifa zitolewe kwa wakati na kwa viongozi husika ili kujua namna ya kukabiliana na tatizo hilo.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *