Viongozi 9 kuchunguzwa baraza la maadili

SEKRETARIETI ya Maadili ya Viongozi wa Umma imepeleka malalamiko kwenye baraza la maadili yanayohusu tuhuma za ukiukwaji wa maadili kwa viongozi wa umma tisa.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana jijini hapa, Kamishna wa Maadili, Jaji Sivangilwa Mwangesi alisema baraza la maadili linatarajia kufanya kikao cha uchunguzi wa kina wa malalamiko hayo.

Baraza hilo litafanya kikao hicho cha uchunguzi wa kina wa malalamiko hayo kwa mujibu wa kanuni ya 11 ya kanuni za maadili ya viongozi wa umma inayohusu mwenendo wa uchunguzi wa malalamiko katika baraza la maadili ya mwaka 2017.

Jaji Mwangesi alisema kikao hicho cha uchunguzi wa kina kitafanyika jijini Dodoma kuanzia Septemba 6 hadi 16, mwaka huu.

Uchunguzi huo wa kina na wa wazi, unafanyika kwa mujibu wa kifungu cha 25 (5) na 29 (6) cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma, sura 398.

Katika kikao hicho cha uchunguzi, wananchi wote mkoani Dodoma na mikoa mingine wanaalikwa kuhudhuria.

Sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma ni taasisi inayojitegemea chini ya ofisi ya rais iliyoanzishwa kwa mujibu wa ibara ya 132 ya Katiba ya mwaka 1977 ili kutekeleza sheria ya maadili ya viongozi wa umma Na. 13 ya mwaka 1995.

Jukumu kubwa la taasisi hiyo ni kuchunguza tabia na mwenendo wa kiongozi yeyote wa umma kwa madhumuni ya kuhakikisha masharti ya sheria ya maadili ya viongozi wa umma yanazingatiwa.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button