WAZIRI wa Nishati, January Makamba amemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano wa viongozi wa dunia unaojadili programu ya Afrika kukabili mabadiliko ya tabianchi.
Mkutano huo unaofanyika Rotterdam, Uholanzi, unalenga kushawishi washirika wa maendeleo, taasisi za kifedha na sekta binafsi na marafiki wa Afrika kuchangia fedha kwenye Programu hiyo ya Afrika ambayo inahitaji Dola za Marekani bilioni 25 ifikapo 2025.
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imechangia Dola za Marekani bilioni 12.5. Mkutano huo unafanyika kama sehemu ya maandalizi Mkutano wa 27 Nchi Wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu Sharm El Sheik, Misri.
January amekutana na viongozi wa dunia, wakuu wa taasisi na mashirika kujadili fursa zikiwamo namna bora ya Tanzania kunufaika na mpango huo utakaoharakisha mipango ya nchi katika kukabili majanga yakiwamo Covid-19, ukame, njaa, ajira kwa vijana na mafuriko.
Mkutano huo uliongozwa na Rais wa Jamhuri ya Senegal na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Macky Sally na Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kituo cha Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (GCA), Ban Ki-Moon.
Septemba 2, mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula alisema Tanzania ipo tayari kushiriki katika jitihada za kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Balozi Mulamula alitoa kauli hiyo Dar es Salaam wakati wa kufunga Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi na Maendeleo ulioandaliwa kwa pamoja na Serikali ya Tanzania na Uingereza na kushirikisha nchi 20.