Viongozi Bandari za Burundi ziarani kujifunza
KIGOMA:Ujumbe wa viongozi wa serikali ya Burundi wanaosimamia uendeshaji wa bandari na usafirishaji majini umeanza ziara ya siku tatu mkoani Kigoma kujifunza na kupata uzoefu kuhusu shughuli za uendeshaji bandari na sheria zinazosimamia usafirishaji salama wa vyombo vya majini.
Ujumbe huo wa watu watano unaongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka ya Bandari na usafirishaji majini wa Burundi, Kanali Biherengende Jean Babtist ambaye amesema kuwa wanaamini ziara yao itakuwa na mafanikio makubwa katika kupata namna mpya itakayosaidia uendeshaji wa bandari na usafirishaji majini nchini Burundi.
Akizungumza katika ufunguzi wa majadiliano ya kupeana taarifa ya namna nchi hizo zinavyoendesha na kusimamia bandari na usafirishaji majini amesema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa kwenye suala hilo hivyo wanamaamini ziara hiyo itawapatia maarifa makubwa.
Amesema kuwa kwa sasa Burundi imeanza kutekeleza mradi mkubwa wa uboreshaji wa bandari ya Bujumbura kwa kuboresha eneo la kuhifadhia makasha na ujenzi wa bandari nyingine mbili karibu na Mpaka wa Tanzania hivyo ziara hiyo inalenga kuwapa watendaji waandamizi wa mamlaka za bandari na usafirishaji majini nchini Burundi ili waweze kupata mafanikio kwenye utendaji wao.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu Wakala wa meli nchini (TASAC),Rajabu Mabamba akizungumza katika mkutano huo amesema kuwa ziara hiyo itawaweka pamoja kuona namna wanaimarisha shughuli za pamoja za usafirishaji majini na sheria zilizopo ili kuona namna ambavyo shughuli za usafirishaji majini zinakuwa salama kwenye ziwa Tanganyika.