MIGOGORO mingi maeneo ya kazi imedaiwa kusababishwa na viongozi kutokana na kutoa lugha za kuudhi kwa watumishi na wateja.
Hayo yamesemwa leo Aprili 27,2023 jijini Dar es Salaam na Afisa Mtendaji Mkuu wa Uongozi Institute, Dokta Kadari Singo katika mkutano wa Jumuia ya Afrika katika masuala ya utawala na uongozi Chapter Tanzania (AAPAM).
Dkt Singo amesema, mwaka jana peke yake walipokea maombi ya kutoa mafunzo kutoka kwenye taasisi 100 kati ya hizo walifanyia kazi maombi 86 kwa kuwanoa viongozi 496,000.
“Fikiria hao ni viongozi tuliwanoa lakini bado malalamiko hayaishi tunaonekana bado hatujafanya kitu, kwa hiyo tunachokifanya sasa tukiletewa maombi tuna ‘diagnosis’ unakuta matatizo ya ndani ya ofisi ni mengi na mengi yanasababishwa na viongozi….; “Unakuta wakati mwingine tatizo sio ‘capacity’ ni mifumo, hivyo wengine tunawarudisha wakamalize kwanza matatizo ya ndani ndio warudi tuwape mafunzo, kama matatizo ya ndani hamjayamaliza hata mpewe mafunzo mwaka mzima hakuna kitakachobadilika.”Amesema
Aidha, amewataka mameneja rasiliamli watu kuacha kuegemea upande mmoja uwe wa uongozi au watumishi na kuwataka kuwa katikati ili wafanye kazi kwa weledi bila kumuonea mtu na kupunguza malalamiko.
Akitolea mfano amesema “Kuna barua moja katibu wa utumishi alinionyesha, yaani kiongozi anaandika kwa hasira unaiona hasira yake kwenye ile barua, ukicheki majibu ya mtumishi nayo amejibu kwa hasira, lakini chanzo cha ule mgogoro ni Meneja Rasilimali Watu ambae aliegemea upande wa uongozi.
“Ukiona sehemu yoyote ukiwa kama kiongozi kuna mgogoro basi jitathmini kwanza wewe mwenyewe, utagundua tu wewe ndio tatizo, kabla ya kuona wenzio ndio tatizo….unakuta mtu kajaza likizo mkuu wake wa kitengo kamruhusu wewe meneja rasilimali watu unaikalia fomu yake au kumkatalia kwa nini? Alihoji na kuongeza
“Kama kuna upungufu mkuu wa kitengo ndio anafahamu, yeye kamruhusu wewe unamuwekea vikwazo ili iweje? Natarajia mafunzo haya yatawabadilisha na kwenda kuleta ufanisi kwenye maofisi yenu.”Alisema