VIONGOZI wa dini na mila wa mkoa wa Rukwa wamepaza sauti wakitaka kujua ni lini serikali itaifanyia mabadiliko Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 waliyosema mapungufu na changamoto zake zinachochea mimba na ndoa za utotoni mkoani mwao na Taifa kwa ujumla.
Viongozi hao wamesema wakati Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 inamtafsiri kuwa ni mtu yoyote mwenye miaka chini ya 18, Sheria ya Ndoa inaruhusu mtoto wa kike chini ya umri huo kuolewa.
Mwaka 2019, Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ilithibitisha uamuzi wa Mahakama Kuu katika kesi ya Rebeca Gyumi ya mwaka 2016 dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali kuwa vifungu vya 13 na 17 vya Sheria ya Ndoa vinavyoruhusu mtoto kuolewa kwa idhini ya wazazi akiwa na miaka 15 na mahakama akiwa na miaka 14 ni vya kibaguzi na ni kinyume na Katiba.
Katika uamuzi huo, Mahakama Kuu iliamua kuwa Sheria ya Ndoa ipitiwe upya ili kuondoa ubaguzi na kukosekana kwa usawa kati ya umri wa chini wa ndoa kwa wavulana na wasichana.
Mahakama ilisema kuwa Kifungu cha 13 na 17 cha Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 kinakwenda kinyume na Ibara ya 12, 13 na 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambayo inatoa haki sawa kwa wote mbele ya sheria.
“Sheria ya sasa inamtaka mwanaume kuoa akiwa na umri wa miaka 18 ambao kikatiba ni mtu mzima, lakini sheria hiyo inaruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa hajafikia utu uzima,” anasema Askofu Ambele Mwaipopo wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Ziwa Tanganyika, Rukwa.
Anasema mkanganyiko huo wa sheria unatoa tafsiri nyingine kwamba mtoto wa kike ni mtu mwenye umri chini ya miaka 14 na wala sio miaka 18 tena.
Anasema kama sheria inamtaja mtoto kama ni mtu mwenye miaka chini ya 18 na inataja haki zake mbalimbali ikiwemo kuendelezwa kielimu basi Sheria ya Ndoa inatoa mwanya au ni kichocheo cha ndoa na mimba za utotoni kwa kuwa inaruhusu mtoto kuolewa akiwa na miaka 14 au 15.
Ili kuondoa mkanganyiko huo, Askofu Mwaipopo anasema serikali haina budi kufanya marekebisho ya haraka ya sheria hiyo ili kuwanusuru watoto wakike wasipoteza haki zao ikiwemo Haki ya Kuendelezwa ambayo kwa mujibu wa Sera ya Maendeleo ya Mtoto Tanzania; maendeleo hayo yanahusiana na mtoto kuwa na kiwango kinachokidhi makuzi kimwili, kiakili, kiroho, kimaadili na kijamii.
Anasema sheria ya Kanisa inatambua mazingira ambayo yanaweka vizuizi kwa watu wakiwemo watoto kufunga ndoa hata hivyo sheria za nchi kwa upande mwingine zinawaweka njiapanda pale ridhaa ya wazazi au amri ya mahakama inapotolewa.
“Ndoa na mimba za utotoni ni moja ya changamoto zinazoukabili mkoa wa Rukwa. Masuala haya ya kuanza uzazi katika umri mdogo yanachukuliwa na jamii yetu kama ya kawaida bila kutafakari madhara yake,” anasema Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Donald Nsoko.
Nsoko anasema takwimu za utafiti wa kidemografia za mwaka 2015 hadi 2016 zinaonesha asilimia 29 ya wanawake wenye miaka kati ya 15 na 19 mkoani humo walikuwa wajawazito au wamezaa.
Anasema utafiti huo mkoani humo unaonesha katika kipindi cha mwaka 2017 hadi 2019 kulikuwa na jumla ya matukio 722 ya wanafunzi kupata mimba ambayo kati yake 171 yalitokea katika shule za msingi na 551 kwa shule za sekondari.
Sheikh wa Mkoa wa Rukwa, Rashid Akilimali anasema; “Kama sheria inasema umri wa mtoto kuolewa ni miaka 18 kwanini tena kiwekwe kifungu kinacholegeza sharti hilo na kuruhusu mtoto huyo kuolewa kwa idhini ya wazazi au kwa amri ya mahakama akiwa na umri chini ya miaka 18.”
Anaiomba serikali iwashirikishe wadau kuona namna nzuri ya kutekeleza mahitaji ya watu yanayotaka umri wa kuoa au kuolewa uwe kuanzia miaka 18.
Huko Kenya, Sheria ya Ndoa Namba 4 ya mwaka 2014 ya nchi hiyo inasema ili kuoa au kuolewa utahitaji kuwa na umri wa miaka 18 au zaidi na si vinginevyo.
Padri Charles Kasuku wa Jimbo Katoliki Sumbawanga anasema muongozo wa jumla wa dini unapinga ndoa za utotoni na kukataza matendo yote ya uzinzi hivyo ni muhimu serikali kupitia bunge lake ikawa na sheria ya ndoa ambayo haikinzani na sheria ya mtoto na haki zake zingine.
Mchungaji Emmanuel Sikazwe wa Kanisa la Morovian Sumbawanga anakumbusha jinsi Sheria ya Ndoa inavyokinzana pia na kanuni za adhabu ambayo imeanisha kwamba ni kosa la ubakaji kwa mtu yoyote kufanya ngono na mtoto chini ya miaka 18 isipokua kama ameolewa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, ACP Shadrack Masija anasema katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2020 kulikuwa na kesi 97 za mimba za utotoni zilizolipotiwa katika wilaya ya Kalembo, Nkasi na Sumbawanga mkoani humo.
Hata hivyo anasema kati ya kesi hizo 97 ni 10 tu ndizo zilizofikishwa mahakamani na kati yake kesi tatu tayari zimekwisha na watuhumiwa wake wametiwa hatiani huku nyingine saba zikiendelea kusikilizwa.
“Kesi 87 hazijafikishwa mahakamani kwasababu mbalimbali ikiwemo walalamikaji au wahanga kutokuwa tayari kutoa ushahidi, makubaliano ya pande mbili na mlalamikaji kumkana mtuhumiwa,” anasema.
Kwa upande wa ndoa za utotoni, Kamanda Masija anasema kesi tatu ziliripotiwa, mbili tayari zimeanza kusikilizwa mahakamani na moja inaendelea kuchunguzwa.
“Hii ni vita kama ilivyo kwenye matukio mengine, tena ni vita kali- vita hivi vitakuwa vyepesi zaidi kama sheria zinazomlinda mtoto hasa wa kike hazitakinzana,” anasema.
Anasema wana Rukwa wameanza kutambua kwamba mimba na ndoa za utotoni ni changamoto kubwa katika jamii yao na wanashirikiana na vyombo vingine ikiwemo Polisi kutoa taarifa zake.
“Tusiishi kutoa taarifa tu za matukio haya, kwa wale wenye ushahidi wa moja kwa moja wa matukio haya wasiogope kutoa ushahidi wao mahakamani ili kesi zake zifike mwisho na watuhumiwa wake watiwe hatiani,” anasema.
Katika kukabiliana na mimba na ndoa za utotoni, mwaka 2020 Mkoa wa Rukwa ulikuja na Mkakati wake wa miaka mitano (Julai 2020 hadi Juni 2025) unaolenga kupunguza au kumaliza kabisa changamoto hiyo.
Shirika la kimataifa la Plan International kwa kushirikiana na shirika la Yes Tz, Rafiki SDO, Rusudeo, PDF na Chuo cha Maendeleo ya Jamii Chala linatekeleza afua tano zinazolenga kuusaidia mkoa huo kuhakikisha ifikapo mwaka 2025, tatizo la mimba na ndoa za utotoni linakuwa historia.
Meneja wa Mradi wa Kupinga Mimba na Ndoa za Utotoni wa shirika la Plan International, Kisasu Sikalwanda anasema moja ya afua hiyo ni ile inayoangazia masuala mazima yanayohusiana na ulinzi na usalama wa mtoto.
“Kwa kupitia afua hii tunaangalia sera, sheria na mikataba mbalimbali inayomlinda mtoto.
Yeyote anayejua kwamba kuna mtoto anafanyiwa ukatili au kutendewa vibaya hana budi kutoa taarifa kuhusu vitendo hivyo kwa ustawi wa jamii, polisi, dawati la jinsia na watoto, ofisi ya serikali za mtaa, timu ya ulinzi na usalama wa mtoto na tasisi au mashirika ya kijamii,” anasema.
Kaimu Mkurugenzi wa shirika Yes Tz, Beatrice Kingu anataja afua zingine zinazolenga kumnusuru mtoto na aina yoyote ya ukatili wa kijinsia ikiwa ni pamoja na mimba na ndoa za utotoni kuwa ni ile inayolenga kuhakikisha mtoto anabaki shule na kusoma akiwa salama.
Zingine ni kumuinua mtoto wa kike na kaya yake kiuchumi, elimu ya afya ya uzazi na makuzi kwa vijana na kuhakikisha mila, desturi na mitizamo inayohatarisha ustawi wa mtoto wa kike inaachwa au kubadilishwa.
“Tukifuata na kuzilinda mila na desturi zetu tatizo la ongezeko la ndoa na mimba za utotoni ambalo ni moja ya changamoto ya kiafya kwa vijana wetu wa kike-litakwisha,” anasema Chifu wa Wafipa, Chifu Malema Sinyangwe.
Chifu Malema anasema; “Mimba za utotoni hazikubaliki katika jamii ya wana Rukwa na ndio maana mila na desturi zetu zinawataka wazee kwa kupitia madarasa ya kimila wawaangalie watoto wanaokaribia kuvunja ungo au kubalee na kuwafunda.”
Anasema mtoto akishakaribia kuvunja ungo, mama aliwajibika kuchunga nyendo zake na hakumruhusu kushirikiana na mabinti watukutu, urafiki wa karibu na wavulana nje ya mambo yanayowahusu kama vijana wa rika moja na kumtahadharisha yanayoweza kumpata iwapo hatazingatia kanuni za kuishi katika hali ya kupevuka mwili.
“Tunataka elimu, mila na desturi na sheria za nchi ziifanye jamii ichukizwe na vitendo vya watoto wao wa kike kuwa na mahusiano ya kingono ambayo wanaamini yatawaharibu mabinti kwa kuwasababishia ujauzito na matatizo mengine ya kiafya,” anasema.
Katika taarifa yake ya Septemba 2022 iliyotolewa na aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro, Wizara ya Katiba na Sheria ilitangaza kuanza kukusanya maoni ya wadau kwa lengo la kufanyia marekebisho sheria hiyo ya ndoa.
Miongoni mwa wadau hao ambao wizara ilitangaza kuanza kukutana nao ni pamoja na kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, wabunge, viongozi wa dini, viongozi wa kimila na makundi mengine katika jamii.
Wakati Umoja wa Mataifa huchukulia ndoa za watu wa chini ya miaka 18 kuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu, takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) za mwaka 2017 zinaonesha Tanzania ni ya tatu katika ukanda wa Afrika Mashiriki kwa kuwa na viwango vya juu vya ndoa za utotoni baada ya Sudani Kusini na Uganda.
Wakati takwimu za Unicef zinaonesha kiwango cha watoto wanaoozwa wakiwa na umri chini ya miaka 18 nchini Tanzania ni asilimia 31, Sudani Kusini ina asilimia 52 na Uganda asilimia 40.
Comments are closed.