Viongozi mbaroni kwa kuuza ardhi

JESHI la Polisi limewakamata viongozi wanne wa vijiji wilayani Handeni, Tanga kwa tuhuma za kuuza ardhi zaidi ya ekari 500 na mbao 1,000, kinyume na utaratibu.

Viongozi hao walikamatwa Novemba 13, kutokana na agizo la Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omar Mgumba alilolitoa kwenye mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za wananchi katika Kijiji cha Kwamsisi ambapo alisema kuwa viongozi hao wametumia madaraka yao vibaya.

Pia mkuu wa mkoa aliagiza kukamatwa kwa wananchi 27 ambao wapo kwenye orodha ya kudaiwa kununua mashamba isivyo halali.

Viongozi waliokamatwa ni Mtendaji wa Kata ya Kwamsisi Erick Chipindula, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kwedikabu, Rajabu Makamba, Mtendaji wa Kijiji cha Kwedikabu, Zahara Sempule pamoja na Ofisa Misitu wa Wilaya ya Handeni, Elinihaki Mdee.

Aidha, mkuu wa mkoa aliiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani humo kutoka na kufuatilia kwa kina tuhuma hizo na kumwasilishia taarifa ofisini kwake.

“Takukuru fuatilieni hili suala lakini polisi kamateni hawa viongozi wote na wapelekeni ndani kwa ajili ya mahojiano zaidi kwani wameshindwa kutumia vizuri nafasi zao za uongozi walizopewa,” alisema.

Hata hivyo, alisema kwa mkoa huo migogoro mingi ya ardhi imesababishwa na wenyeviti wa vijiji pamoja na watendaji kushiriki katika kuuza maeneo kiholela bila ya kufuata utaratibu uliopo.

Wakati wa kuwasilisha kero kwa mkuu wa mkoa, mkazi wa Kwamsisi, Bakari Ramadhani alisema kata hiyo kwa sasa haina maeneo ya ardhi kwani viongozi hao wameuza hadi maeneo ya serikali na hakuna hatua zilizochukuliwa.

“Hoja yangu ni kwamba viongozi wetu wameuza maeneo ya ardhi lakini licha ya kupeleka taarifa kwenye ngazi husika hakuna hatua iliyochukuliwa, hivyo naamini ujio wako mkuu wa mkoa utaweza kutusaidia juu ya suala hili,” alisema Ramadhani.

Habari Zifananazo

Back to top button