Viongozi Urusi wataka hukumu ya kifo kwa magaidi

MOSCOW, Urusi: VIONGOZI mbalimbali katika serikali ya Urusi chini ya Rais Vladimir Putin wametoa pendekezo la kurudishwa kwa sheria ya hukumu ya kifo kwa wahusika wote walioshiriki shambulio la kigaidi katika Ukumbi wa Jiji la Crocus huko Moscow siku ya Ijumaa.

Katika shambulio hilo la kigaidi kutokea nchini Urusi ndani ya miaka 20 takriban watu 115 waliuawa na 145 wamejeruhiwa.

Naibu Mkuu wa Kamati ya Usalama wa Jimbo la Duma, Yury Afonin, amesema kwamba ni muhimu kurudisha hukumu ya kifo kwa ajili ya wahusika wa tukio hilo baya la kigaidi.

Advertisement

Naye Rais wa zamani wa Urusi Dmitry Medvedev, ambaye sasa ni Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Urusi, ametoa wito kwamba magaidi waliohusika na shambulio hilo la kigaidi na watakaogundulika kusaidia magaidi hao waangamizwe, wauawe wote.

Wanaume wanne, wanaodhaniwa kuwa asili ya Tajikistan, wameshtakiwa kwa kutekeleza shambulizi hilo na wamekiri kuhusika na tukio hilo.

Wanaume hao walionekana kupigwa walipofika katika Mahakama ya Wilaya ya Basmanny katika mji mkuu wa nchi hiyo Jumapili iliyopita na video kusambazwa mtandaoni ikionyesha mmoja wa wanaume hao akiwa amekatwa sehemu ya sikio.

Kundi la Islamic State limedai kuhusika na shambulio hilo. Warusi nchini kote wameendelea kuomboleza wapendwa wao waliopoteza maisha katika tukio hilo.