‘Viongozi wa dini himizeni maadili’

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga, kimewaomba viongozi wa dini na wazee kuisaidia serikali kwenye changamoto ya mmonyoko wa maadili, ili nchi iendelee kuwa na amani na jamii yenye hofu ya mungu.

Ombi hilo limetolewa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdulrahman, wakati wa kikao chake na wazee wa Mkoa wa Tanga, ambapo amesema kuwa iwapo watahimiza maadili nchi itabaki kuwa salama.

“Niwaombe wazee na viongozi wa dini isaidie serikali katika suala zima la mmonyoko wa maadili, ili kuweza kuwa na Taifa lenye watu wenye uadilifu na wacha Mungu,”amesema Mwenyekiti.

Amesema kuwa katika uongozi wake ndani ya chama hicho katika kipindi cha miaka mitano atahakikisha wazee anashirikiana nao bega kwa bega, ili kuweza kuchota hekima na busara zao.

Akizungumza kwa niaba ya wazee Meya Mstaafu wa Jiji la Tanga, Kassim Kisauji alisema kuwa kasi ya utendaji kazi ya kiongozi huyo wa chama utaweza kusaidia kuimarisha chama hicho.

“Nikuombe Mwenyekiti imarisha chama hiki kuanzia ngazi za Wilaya hadi Mkoa, ili tuweze kufanya vizuri kwenye chaguzi zinazokuja, ” amesema Kisauji.

 

Habari Zifananazo

Back to top button