VIONGOZI wa dini watalazimika kurudi ‘shule’ ya maadili, ili kukabiliana na tatizo la mmomonyoko wa maadili unaoshamiri nchini.
Hatua hiyo inatokana na kuongezeka kwa vitendo vya viovu vikiwemo ushoga, ubakaji, ulawiti, huku baadhi ya viongozi wa dini wakihusishwa kwa namna moja au nyingine na vitendo hivyo.
Kauli hiyo imetolewa mbele ya waandishi wa habari leo, Oktoba 12, 2022, jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Taasisi ya Islamic Education Panel (IEP), Mohamed Kassim, wakati akitangaza matokeo ya mtihani wa Elimu ya Dini ya Kiislamu wa darasa la saba uliofanyika Septemba mwaka huu.
Kiongozi huyo amesema, vitendo vya ukatili kwa jamii nzima vinashamiri na kwamba, kitu kibaya zaidi ni walimu na viongozi wa dini kutumbukia kwenye vitendo hivyo, kufikishwa mahakamani na wengine kufungwa.
“Viongozi wa dini wanabaki kuwa wanaadamu kama walivyo wengine, wanaweza kukosa kama ilivyo kwa wengine. Pia wanaweza kuchukuliwa hatua za kisheria kwa makosa kama wanavyochukuwa wanadamu wengine.
‘‘Isipokuwa tu ni jambo la kusikitisha kwa mtu ambaye ulimtegemea ndiye awe mwalimu wa kusimamia maadili, yeye akakosa maadili hayo au akawa msimamizi mbaya wa maadili hayo,’’ amesema Mohammed na kuongeza:
“Tunayo makundi yanayotuunganisha viongozi wa dini, ambapo tumeanza kufanya vikao, ili kufanya kila watu katika eneo lao kuweza kushughulika na ukosefu wa maadili wa watendaji na viongozi wa dini kwenye eneo lao.’’
Amesema taasisi hiyo imepewa kazi ya kutoa semina elekezi kwa viongozi wa dini, shuleni, madrasa na maimamu, ili kuzungumzia kuvunjika kwa maadili na chanzo chake, kisha kuchukua njia muafaka kukabiliana na tatizo hilo.
Amesema viongozi wa dini nchini ambao wamekuwa wakitumika kuwafundisha watoto maadili ya dini, watalazimika kufundishwa tena maadili ya dini, ili kusaida kupunguza vitendo vya ukatili.
Akizungumzia matokeo ya Darasa la Saba katika Elimu ya Dini ya Kiislam mwaka huu amesema, jumla ya shule 3,710 katika mikoa 25 na Halmashauri 151 zilishiriki kufanya mtihani huo.
“Watainiwa waliosajiliwa walikuwa 163,143 na waliofanya mtihani walikuwa 142,522 sawa na asilimia 87.36, huku watahiniwa 20,621 wakishindwa kufanya mtihani huo kutokana na sababu mbalimbali.
“Idadi ya ya watahiniwa waliofaulu kwa kupata madaraja A hadi C ni 95,166 sawa na asilimia 66.77 ya watahiniwa wote, watahiniwa waliopata daraja D na E ni 47,356 sawa na asilimia 33.23 ya watahiniwa wote,” amesema Kassim.
Upande wake Amir Mkuu Baraza Kuu la Jumiiya ya Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Mussa Kundecha amesema, wanafunzi 3,567 wamefanya vizuri kwa kupata ufaulu wa alama A katika mtihani huo na kwamba ufaulu huo umeenda vizuri ikilinganishwa na mwaka jana.
“Shule 10 bora kwa kitaifa katika kundi la shule zenye watainiwa 20 au zaidi namba moja ni Mumtaaz ya Mwanza, Istiqaama ya Tabora, Rahma ya Dodoma, Algebra Islamic ya Dar es Salaam, Dumila ya Morogoro, Islamia ya Mwanza, Hedaru ya Kilimanjaro, Daarul Arqam, Mbagala Islamic na Maarifa Islamic zote za Dar es Salam,” amesema Sheikh Kundecha.