Viongozi wa dini Morogoro wakubali mabadiliko sheria ya ndoa
VIONGOZI wa dini wameungana na serikali katika mabadiliko ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971. Wamesema sheria hiyo inawanyima haki watoto wa kike kutimiza ndoto zao kwa kujikita wakitengeneza familia wakiwa na umri mdogo.
Askofu wa Kanisa la Kiinjili Kilutheli Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Morogoro, Jacob Mameo Ole Paul, amesema hayo katika maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Kike Duniani iliyoandaliwa na Mradi wa Hapana Marefu yasiyo na Mwisho, unaotekelezwa na C-Sema, Amani Girls kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU).
“Sisi viongozi wa dini tuko mstari wa mbele katika mabadiliko ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971,ndoa za utotoni hazikubaliki.” amesema Askofu Mameo.
Askofu Mameo ameishauri serikali kuendelea na mchakato wa mabadiliko ya sheria hiyo ili kuwezesha kutengeneza mazingira rafiki kwa watoto wakike mtoto kuweza kutimiza ndoto zao.
Askofu Mameo ameishauri jamii kuacha tabia ya kubadilisha mazao na binadamu kwa lengo la kuolewa na kwamba watoto wa kike waachwe wasome watimize ndoto zao zitakazowawezesha kulitumikia vyema taifa.
“Watoto wakike hapaswi kuuzwa kama mazao,kwani wana haki ya kupata haki zote ndani ya jamii ikiwemo elimu.” amesema Askofu Mameo.
Naye Sheikh wa Mkoa wa Morogoro, Twaha Kilango amesema ukatili wa kijinsia umeteketeza jamii kubwa ya watanzania,hivyo ifikie wakati tuungane pamoja na kuweka nguvu katika kutokomeza ukatili wa kijinisia hususani kupinga ndoa za utotoni katika jamii zetu.
“Tushikamane, tushirikiane na kupaza sauti katika kutokomeza ukatili kwa watoto wetu wa kike, wakati unabadilika na sisi tunapaswa kubalika, na tutumie viongozi wa dini katika kuelimisha jamii kwa uwazi ili kuibadilisha iondokane na mitazamo ambayo sio sahihi.”amesema Sheikh Kilango.
Naye chifu wa kabila la Kimasai, Kashu Moreto amesifu namna jamii za kifugaji zinavyobadilika kwa kuondokana na mila kandamizi hasa kwa wanawake na watoto wakike.
Amesema mabadiliko hayo yamechangiwa na elimu ambayo inayotolewa kwenye makanisa, misikitini na kwenye jamii inayohumiza wazazi kuwapeleka watoto shule huku akiwataka wazazi kukaa karibu na watoto kujua changamoto zao.
Kwa upande wake kiongozi mkuu wa mradi huo uliopo ndani ya kanisa hilo, Patricia Mwaikenda amesema mradi umekijita katika kufanya mabadiliko katika mila, desturi potofu ndani ya jamii ambazo zinamkandamiza mtoto wa kike kushindwa kutimiza malengo yake.
Mwaikenda ametaja malengo matatu ya mradi huo ni kuwajengea uwezo watoto wa kike kuweza kujitambua na kutoa taarifa pindi wanapofanyiwa ukatili, elimu kwa viongozi wa dini na utetezi wa mabadiliko ya sera na sheria ikiwemo sheria ya ndoa ya mwaka 1971.
Awali, baadhi ya watoto wakike walioshiriki maadhimisho hayo kwa nyakati tofauti wameeleza namna wanavyokabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukatili wa kijinsia nyumbani, shuleni na mitaani.
Wamesema pia baadhi yao kunyimwa fursa sawa ya kupata elimu ili kutimiza ndoto zao, kutothaminiwa hata kufikia hatua ya kulinganishwa thamani na ng’ombe, na kulazimishwa kuolewa katika umri mdogo ili wazazi waweze kupata mali hususani ng’ombe.
Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 haitoi utetezi wa haki ya mtoto wa kike kwa kuwa inahalalisha mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri wa miaka 14 kwa ridhaa ya wazazi.