Viongozi wa dini watakiwa kulea vijana katika maadili

MAKAMU wa Rais, Dk Phillip Mpango amewataka viongozi wa dini nchini kuwafundisha na kulea vijana katika maadili mema na wathamini kufanya kazi kihalali.

Dk Mpango alisema hayo Jumapili katika hotuba yake iliyosomwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angeline Mabula katika Jubilee ya miaka 25 ya Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni Kibiti na sherehe za kutaburuku kanisa na altare iliyofanyika Kibiti mkoani Pwani.

Alisema, kuna mmomonyoko wa maadili katika jamii, vitendo viovu na mambo yasiyompendeza Mungu kuzidi kuongezeka na sasa yanakuwa habari za kila siku na wakati mwingine huonekana ni kawaida.

Dk Mpango alisema kushuka kwa maadili ni jambo lenye athari mbaya kwa jamii na kunachangia kurudisha nyuma juhudi za kujiletea maendeleo nchini.

Kupitia hotuba ya Makamu wa Rais, Dk Mabula alisema, anaamini watu wakiwemo viongozi wa serikali na wa vyama vya siasa wakishika mafundisho ya dini na kuwa na hofu ya Mungu maovu yatapungua.

Aliomba viongozi wa dini wasaidie kulea taifa katika kimaadili na kuweka mkazo zaidi kwa vijana kwa kuwa ni waathirika wakuu wa maovu yanayotendeka na pia ni viongozi wa kesho.

Pia alihimiza usafi na utunzaji mazingira na akaomba viongozi wa Kanisa Katoliki na madhehebu mengine ya dini wapaze sauti kuhamasisha, ulinzi na uhifadhi wa mazingira.

“Niwaombe ninyi mlio mawakala wa mwenyezi Mungu hapa duniani muwaongoze waumini na kuwahimiza kuitunza ekolojia ya nchi yetu nzuri kwa kutunza misitu na vyanzo vya maji, kupanda miti na kufanya usafi wa mazingira wakati wote” alisema Dk Mpango.

Aliomba viongozi wa dini wakemee mimba na ndoa za utotoni kwa kuwa ni kinyume cha sheria na maadili na suala hilo linawanyima fursa watoto wa kike kusoma na kufikia malengo yao sanjari na kusababisha matatizo ya fistula.

Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Jude Thaddaeus Ruwa’ichi aliwapongeza wana Kibiti kwa kuwa na kanisa lililokamilika.

Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema kanisa hilo limejengwa kwa miaka 11 na akampongeza

padri wa Parokia ya Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni Kibiti, Christian Lupindu kwa kujituma.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button