DAR ES SALAAM; VIONGOZI wa mila na desturi nchini wametakiwa kushirikiana katika kuwahamasisha Watanzania kutumia takwimu zilizotolewa baada ya Sensa ya Watu na Makazi kuleta mwelekeo unatarajiwa kimaendeleo.
Akifungua mafunzo ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya Sensa ya Watu na makazi kwa viongozi wa mila na desturi Dar es Salaam leo Katibu Mkuu, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa alisema matokeo ya Sensa ni muhimu kwani ndiyo dira inayoongoza kufanya maamuzi ya msingi na kujibu changamoto zinazowakabili wananchi.
Alisema matokeo hayo yatawasaidia viongozi hao kujua jamii waliyonayo na jinsi ya kukaa nayo katika kupanga mipango ya maendeleo.
“Niwapongeze sana machifu kwa kuwa sehemu ya serikali kusukuma ajenda mbalimbali za kimaendeleo, naamini mafunzo haya yatawasaidia kufahamu hali halisi na kufanya maamuzi katika kutoa ushauri,”alisema.
Kamisama wa Sensa ya Watu na Makazi ,Anne Makinda alisema ni vizuri viongozi hao wakajua matokeo kwani wanataka Watanzania wote wazungumze lugha moja.
Amesema matokeo hayo ni ya kihistoria kwa sababu hakuna nchi iliyofanikiwa katika Sensa kama Tanzania kwa kuhesabu watu wengi.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Machifu nchini, Antonia Sangalali alisema machifu wapo tayari kushiriki kikamilifu kama walivyofanya kipindi cha Sensa ya Watu na Makazi.