Viongozi wa michezo wafundwa Utawala Bora

VIONGOZI wa michezo nchini wametakiwa kuwa na kanuni za wazi za fedha katika vyama au mashirikisho yao, ili kuweka uwazi kwa wadau kuhusu mapato na matumizi ya fedha.
Hayo yameelezwa na Mwanasheria Ibrahim Mkwawa katika warsha ya siku mbili ya Utawala Bora kwa viongozi wa mashirikisho na vyama vya michezo nchini iliyoandaliwa na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) iliyoanza Desemba 11, 2022.
Mkwawa aliyewahi kuwa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezoni nchini, anasema kuwa kuwa mashirikisho ya kimataifa yanayataka mashirikisho ya kitaifa kuwa na kanuni za wazi za fedha.
Alisema kuwa mashirikisho hayo ya michezo ya kimataifa yanataka vyama vya kitaifa lazima kuwa na watia saini zaidi ya mmoja, ili kupunguza matumizi mabaya ya fedha.
Mkwawa pia amesema kuwa utawala bora ni muhimu sana katika uongozi wa michezo, kwani hata wafadhili wamekuwa makini sana na uwepo wa kanuni za fedha ili waweze kutoa fedha zao.
Naye Makamu wa Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Henry Tandau amesema kuwa mashirikisho ya michezo pia yanatakiwa kuwa na mipango au utaratibu wa vita dhidi ya dawa zinazopigwa marufuku michezoni (doping).
Anasema suala hilo kwa sasa limekuwa linapigwa vita dunia nzima kutokana na athari zake, ikiwemo kuharibu afya ya wachezaji wanaotumia dawa hizo, na kwa wanawake wamekuwa hata wakipoteza maumbo au maumbile yao ya asili na kuwa kama wanaume.
Pia amezungumzia umuhimu wa vyama kuwawekea bima za afya au ajali wachezaji wao pamoja na vifaa wanavyotumia ili kujikinga na majanga mbalimbali.