WAKUU wa wilaya nchini wameagizwa kuwachukulia hatua za kisheria wenyeviti na watendaji wote wa vijiji na ambao ni chanzo cha migogoro ya wakulima na wafugaji na ikiwezekana wawaweke ndani.
Agizo hilo limetolewa leo na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Daniel Chongolo akiwa katika Kijiji cha Itete,wilayani hapa akiendelea na ziara yake mkoani Morogoro kukagua utekelezaji wa ilani ya chama na miradi ya maendeleo ya umma.
Akiwa katika Shina namba 5, katika kijiji hicho,wananchi walitoa kero zao na kusema migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji imesababisha wakulima kuharibiwa mazao yao na mifugo ya wafugaji ambao huingiza mifugo kijijini bila kufuata utaratibu.
Akizungumzia suala hilo,Chongolo amesema baadhi ya wenyeviti na watendaji wa vijiji wanahusika kwenye migogoro hiyo kwa kupokea rushwa kutoka kwa wafugaji ili kuruhusu mifugo kuingia katika vijiji na kuharibu maeneo ya kilimo na kula mazao yao.
“Niwaagize nyie wakuu wa wilaya wachukulieni hatua na ikiwezekana muwasweke ndani watendaji na wenyeviti wa vijiji wanaoshiriki kuvunja sheria kwa kuruhusu mifugo kuingia vijijini bila vibali na kuleta migogoro na wakulima,”amesema Chongolo.