Viongozi wananufaika migogoro ya ardhi

MOROGORO; Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amesema migogoro mingi ya ardhi ndani ya mkoa huo ina sura mbaya,ni ya kutengenezwa na wapo watu wakiwemo viongozi  wananufaika na migogoro hiyo kimyakimya.

Hivyo amewaagiza wakuu wa wilaya kufanya tathimini ya migogoro ya ardhi katika maeneo yao ambayo wataisimamia na itaratibiwa na wakurugenzi  wa kila halmashauri, ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Malima ametoa maagizo hayo kwenye  kikao na wakuu hao wailaya na wakurugenzi,  ambacho kilihusu mwelekeo wa mkoa baada ya yeye  kufanya ziara kila wilaya na kuona shughuli  mbalimbali ndani ya kipindi cha miezi mitatu tangu alipokabidhiwa mkoa huo.

“ Nimepata heshima ya  kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, nimepata   muda wa kuona mambo mbalimbali  nimefanya ziara ya kujitambulisha  na nyingine  ya kupitia hoja za CAG na tulikubaliana mambo kadhaa na  kukaa kwangu kwa miezi hii mitatu ,tunaona bado hatuendi vizuri sana, “  amesema  Malima.

Ameyataja mambo matatu ambayo hayaendi vizuri sana ni kuwepo kwa migogoro ya ardhi iliyokithiri , migogoro ya wafugaji na wakulima pamoja na migogoro baina ya  viongozi wenyewe kwa wenyewe.

“ Lakini katika hili  lazima tukubaliane ya kwamba migogoro  ya ardhi ya Morogoro mingi ni ya kujitakia wenyewe …nimejipa muda wa miezi mitatu kukaa kama mkuu wa mkoa wa Morogoro na kuyaelewa na kuyasoma, lakini mingi ni migogoro ya kujitakia, “ amesema.

Amesema kuwa, wapo  viongozi kwenye ngazi za vitongoji ,  vijiji  na kata  ambao ni chanzo cha kutengeneza hiyo migogoro.

“ Nataka niseme kwa kweli kati hili masuala ya migogoro ya ardhi , nimeliangalia  na nimebaini migogoro mingi ni ya kutegeneza  hasa kwa viongozi sisi wenyewe, “ amesema  Malima

Kutokana na uzito wa jambo hilo amemtaka   kila mkuu wa wilaya na kamati yake ya usalama  kwenda kufanya tathimini ya migogoro ya ardhi katika  maeneo yao  na kuwasilisha taarifa kwake ili hatua ziweze kuchukuliwa.

“ Tunakuwa na migogoro ambayo inatengenezwa na watu , harafu inasambaa na kuleta sifa mbaya kwenye mkoa wetu wa Morogoro “ amesema  Malima.

Habari Zifananazo

3 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button