Viongozi wapongeza utendaji mamlaka za maji

WAKUU wa wilaya, wabunge na viongozi wa vyama vya siasa wamepongeza hatua ya Wizara ya Maji kutenga bajeti na kuleta fedha za utekelezaji wa miradi ya maji kwa wakati huku wakipongeza utendaji kazi wa mamlaka za maji mjini na vijinini kwa kutekeleza miradi ya maji yenye thamani sawa na fedha zinazotolewa.

Waziri wa Maji, Juma Aweso amefanya ziara ya kukagua, kutembelea na kuzindua miradi ya maji katika Wilaya za Biharamulo, Bukoba, Missenyi, Kyerwa, Karagwe, na Ngara ambapo ameridhishwa na kupongeza jitihada za mamlaka za maji ambazo ni Buwasa na RUWASA kwa upande wa vijijini.

Advertisement

Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo, ACP Advera Bulinda alisema katika miaka miwili iliyopita Wilaya ya Biharamulo vijiji vilivyokuwa na maji safi na salama ni vinne lakini mpaka sasa vijiji vyenye maji safi na  salama wilaya hiyo vimefikia 24.

Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Kanali Wilson Sakulo alisema miaka miwili iliyopita hakukuwa na kijiji kilichokuwa kinatumia maji ya bomba wilayani Missenyi na kwa sasa vijiji 44 vimepata huduma ya maji kati ya vijiji 77 huku vijiji vingine vikiwa katika bajeti ya kupata miradi ya maji mwaka 2023/2024 ambapo mbunge wa Jimbo la Nkenge Frolent Kyombo alisema kuwa kwa sasa bajeti ya maji imeongezeka mara dufu kutoka Sh bilioni 1 mwaka 2020 hadi Sh bilioni 9.

Mbunge wa Jimbo la Kyerwa, Inocent Bilakwate alisema kuwa watumishi wengi waliopangiwa kazi wilayani hapo waliacha kazi na wengine kuhama kwa ukosefu wa maji safi na salama lakini sasa upatikanaji wa maji ni asilimia 61 kutoka asilimia 36 .4 mwaka 2020 huku bajeti ya maji ikiwa imefikia Sh bilioni 12 kwa mwaka 2023/2024 kutoka milioni 900 mwaka 2020.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema: “Nimeridhishwa na Pongezi walizotoa viongozi wa vyama vya siasa wabunge na wananchi ikiwemo wakuu wa wilaya ,nimefurahi,lakini katika kufikia adhima ya upatikanaji wa maji vijijini asilimia 85, na 95 mjini kwa mwaka 2025 ni lazima tuwe na vyanzo vya kudumu hivyo Mkoa wa Kagera hauna umasikini wa vyanzo vya maji kwani Kuna mito mikubwa Kama mto Kagera, Ziwa Victoria kilichobaki ni nyie wataalamu kuleta mpango  mkakati wa kutoa maji katika vyanzo hivi na kupeleka kwa wananchi hivyo changamkeni.”

Katika kuhitimisha ziara yake aliziomba mamlaka za maji  kuhakikisha wanafanya ushirikishi wa miradi katika jamii kwani jamii ikishirikishwa ni rahisi kutunza miradi hiyo kuliko kuona inatekelezwa katika vijiji vyao bila Taarifa.

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *