UJENZI wa reli ya kisasa ya SGR unategemewa kuchochea maendeleo katika sekta ya kilimo, biashara, madini na viwanda huku serikali ikiainisha manufaa makubwa ambayo nchi imeanza kushuhudia kutokana na utekelezaji wake.
Akizungumza na HabariLEO, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa alitaja manufaa hayo ni pamoja na kutoa fursa za ajira ya moja kwa moja kwa Watanzania wapatao 16,000 na ajira zisizo rasmi zaidi ya 80,000.
Kadogosa alisema awamu ya kwanza ya SGR inajumuisha ujenzi wa mtandao wa reli wenye kilometa 1,219 inayoanzia Dar es Salaam hadi Mwanza huku kukiwa na vipande vitano ambavyo vimefikia hatua mbalimbali za utekelezaji.
Dar-Morogoro
Reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro inajumuisha urefu wa kilometa 300 na njia kuu ni kilometa 205 na njia za kupishana huku kukiwa na stesheni sita. Nazo ni Dar es Salaam, Pugu, Soga, Ruvu, Ngerengere, Morogoro na kituo cha karakana na treni za mizigo kilichopo Kwala mkoani Pwani.
Mradi unatekelezwa na mkandarasi Yapi Merkezi na ujenzi wa kipande hiki umefika 97.
19 na unatekelezwa kwa thamani ya Sh trilioni 2.7.
Morogoro – Makutupora
Alisema kipande kina kilometa 422 huku njia kuu ikiwa ni kilometa 336 na njia za kupishana kilometa 86. Zipo stesheni nane ambazo ni Mkata, Kilosa, Kidete, Gulwe, Igandu, Dodoma, Bahi, Makutupora na kituo cha karakana na treni za mizigo kilichopo Ihumwa mkoani Dodoma.
Mradi unatekelezwa na mkandarasi Yapi Merkezi na ujenzi umefika asilimia 87.05 huku kipande hicho kikijengwa kwa gharama ya Sh trilioni 4.4.
Makutupora-Tabora
Kipande hiki cha tatu kina urefu wa kilometa 368, njia kuu ni kilometa 294 na njia za kupishana kilometa 74 huku kikiwa na stesheni saba za Manyoni, Itigi, Tura, Malongwe, Goweko, Igalula na Tabora.
Mradi unatekelezwa na kampuni ya Yapi Merkezi kwa thamani ya dola za Marekani bilioni 1.908 sawa na Sh trilioni 4.406. Kazi za awali na usanifu wa kina wa njia unaendelea. Muda wa ujenzi ni miezi 46 ikijumlisha muda wa majaribio.
Tabora-Isaka
Kipande cha nne kutoka Tabora hadi Isaka, kina kilometa 165, njia kuu ni kilometa 130 na njia za kupishana kilometa 35. Kipande hiki kina stesheni tatu za Nzubuka, Ipala Bukene-Tabora.
Mradi unatekelezwa na mkandarasi Yapi Merkezi kwa gharama ya dola za Marekani milioni 900.
1 sawa na Sh trilioni 2.094 na muda wa utekelezaji ni miezi 42 ikijumlisha muda wa majaribio wa miezi sita.
Isaka-Mwanza
Kipande cha tano ni cha Isaka hadi Mwanza chenye urefu wa kilometa 348. Njia kuu ni kilometa 249 na njia za kupishana kilometa 92 na stesheni nane za Isaka, Bukene, Shinyanga, Seke, Malampaka, Bukwimba, Mantare, Mwanza Central na kituo cha karakana na treni za mizigo kilichopo Fela mkoani Mwanza.
Mradi unatekelezwa kwa ubia kati ya kampuni ya CCECC na CRCC kutoka China na ujenzi wa kipande hiki umefika asilimia tisa na thamani ya mradi ni Sh trilioni 3.1.
Ajira lukuki
Alisema wafanyakazi 378 wamehudhuria mafunzo mbalimbali ndani na nje ya nchi yakiwamo ya usalama wa reli, mafunzo elekezi katika utumishi wa umma yaliyolenga kuwajengea uwezo wafanyakazi kuhusu kanuni na taratibu za utumishi wa umma na mafunzo mengine ya kitaaluma.
Aidha, mradi huo wa SGR unaelezewa kuwa umetoa fursa za ajira ya moja kwa moja kwa Watanzania wapatao 16,000 na ajira zisizo rasmi zaidi ya 80,000.
Kwa mujibu wa Kadogosa, katika kutekeleza mradi wa SGR kwa vipande vyote vitano, wamezingatia matumizi ya rasilimali na bidhaa kutoka ndani ya nchi. Kwa kiwango kikubwa vifaa, malighafi na bidhaa nyingine zinazotumika katika mradi wa SGR zinatoka nchini.
Alisema kwa upande wa malighafi na vifaa vya ujenzi vinavyotumika katika mradi ni pamoja na saruji inayotoka nchini na inakadiriwa zaidi ya mifuko milioni tisa ya saruji itatumika katika mradi wa SGR.
Pia nondo zinazotumika katika mradi zinatoka nchini na zaidi ya kilogramu milioni 115 zitatumika wakati mataruma zaidi ya 1,200,500 yatazalishwa kwa ajili ya mradi wa SGR.
“Pia mchanga na kokoto ni miongoni mwa malighafi zinazotoka nchini kwa ajili ya mradi ambapo wakandarasi wazawa zaidi ya 1,600 wanafanya kazi mbalimbali ikiwemo kuleta malighafi hizo katika mradi.”
Bidhaa nyingine zinazotumika kila mwezi kutoka viwanda vya ndani ni nyama ya ng’ombe zaidi ya kilogramu 52,324 kwa mwezi, nyama ya kuku kilogramu 36,421, mayai 131,213, maziwa lita 19,141, maji lita 1,710,186, sukari kilogramu 11,972, mchele kilogramu 98,538 na unga kilogramu 38,745 hutumika kila mwezi kutoka viwanda vya ndani.
Manufaa zaidi
Kadogosa alisema faida za mradi ni kuongeza usafirishaji wa mizigo ambapo reli itabeba mzigo wa mpaka tani 10,000 kwa mkupuo sawa na uwezo wa malori 500 ya mizigo na kuongeza ajira kwa wazawa katika sekta na fani mbalimbali.
Pia uokoaji wa muda kwa usafiri wa abiria na mizigo utasaidia kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla kwa kuongeza muda wa uzalishaji.
Kutakuwa na uboreshaji wa huduma za kijamii ikihusisha ujenzi wa shule, vituo vya afya na ujenzi wa barabara katika maeneo yanayopitiwa na mradi.
Manufaa mengine ni kuchochea maendeleo katika sekta ya kilimo, biashara, madini na viwanda hususani katika maeneo ambako reli hiyo inapita pamoja na nchi jirani hasa Rwanda, Burundi, Uganda, Kenya na DRC.
Vilevile kutakuwa na faida za kiuchumi kwenye sekta ya usafirishaji hasa kupunguza gharama za mara kwa mara za matengenezo ya barabara.
Ilani yatekelezwa
Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kipindi cha miaka mitano, imeelekeza serikali iendelee kuwekeza katika miundombinu ya kimkakati ya reli.
Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano (2021/2022-2025/2026) unaelekeza uboreshaji na uendelezaji wa miundombinu ya reli ili kurahisisha shughuli za kiuchumi zikiwemo za kukuza biashara ndani na nje ya nchi kwa kuunganisha mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Kigoma, Katavi na nchi zisizokuwa na bandari za Rwanda, Burundi, DRC na Uganda.
Pia unaelekeza ukamilishaji wa ujenzi mtandao wa SGR yenye urefu wa kilometa 1,219 kwa lengo la kuongeza kiwango cha usafirishaji wa shehena za mizigo hadi kufikia tani milioni 2.2 na usafirishaji wa abiria hadi kufikia watu milioni 2.3.