Vipindi vya Ubongo vyafikia familia mil 32

KAMPUNI ya uzalishaji vipindi vya elimu burudani ya Ubongo iliyoanzia nchini imetimiza miaka kumi huku ikifikia familia milioni 32 Afrika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Ubongo, Mwasi Wilmore amesema kampuni hiyo sasa inajivunia kuleta mabadiliko katika elimu na kuwawezesha mamilioni ya watoto Afrika.

“Kupitia mkusanyiko wa programu za elimu zinazovutia ikiwemo Akili and Me, Ubongo Kids, bila kusahau Nuzo and Namia iliyoanzishwa hivi karibuni, Ubongo imeendelea kuwa kinara katika nyanja ya ubunifu katika ujifunzaji wa watoto,” amesema na kuongeza:

Advertisement

“Kupitia teknolojia mbalimbali kama vile televisheni, redio na simu za mkononi, Ubongo imeweza kufikia familia zaidi ya milioni 32 barani Afrika na kufanya athari kubwa katika sekta ya elimu ya bara hili.”

Amesema utafiti huru uliochunguza programu za Ubongo umeonesha mara kwa mara matokeo mazuri kama vile  kuboresha utayari wa mtoto kuanza shule na viwango vya ujifunzaji na kuchangia mabadiliko chanya ya kijamii na kitabia kwa watoto na walezi wao.

“Programu za Ubongo zilizojaa ubunifu na zenye kusisimua, zinawawezesha watoto kupata maarifa na stadi muhimu zinazowasaidia kubadili maisha yao na jamii zao kwa ujumla.”

“Huu ni ushuhuda wa kazi ngumu, uaminifu na shauku ya timu yetu, washirika wetu, na wafuasi wetu ambao wameamini katika lengo letu na kuchangia mafanikio yetu. Pamoja, tumeweza kufanya mabadiliko makubwa katika elimu Afrika, na tuna azma ya kuendelea na safari yetu ya kuleta mabadiliko katika ujifunzaji wa watoto kwa vizazi vijavyo,” alisema.

Katika kuadhimisha miaka hiyo 10 amesema kutakuwa na tukio litakalojumuisha hotuba na mawasilisho yakionesha safari na athari za programu za Ubongo.

“Tukiangalia miaka kumi ijayo, tunatazamia kusimama imara katika dhamira yetu ya kuwafikia watoto wengi zaidi, tukitumia nguvu ya elimu burudani kuwawezesha kufikia uwezo wao na kujenga mustakabali bora wa Bara la Afrika,” alisema.

Muasisi wa kampuni ya uzalishaji vipindi vya elimu burudani ya Ubongo, Cleng’a Ng’atigwa (katikati) akizungumza kwenye hafla ya miaka 10 toka kuanzishwa kwa kampuni hiyo, Dar es Salaam leo. Kushoto ni Mkurugenzi wa Mawasiliano na Maendeleo, Iman Lipumba na mwigizaji Mohamed Kingala ‘Mau Zumo’. (Picha na Rahel Pallangyo).

Tangu kuanzishwa kwake Julai 2013 mkoani Dar es Salaam, Ubongo imejikita katika kutengeneza maudhui ya elimu yenye kufurahisha, kuelimisha na yenye kuzingatia lugha na tamaduni za Kiafrika zinazomfanya mtoto apende kujifunza.

2 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *