“Visa vikali vya kusisimua”

ANAUJUA ubora wake hasa katika suala la uandishi wa visa vikali vya kusisimua. Kupitia maandishi yake ameweza kutengeneza mashabiki lukuki kutoka kila kona ya dunia, kwa kutumia kalamu yake tu.

Visa vya kusisimua na kutisha ndivyo anavyovihusudu sana, ndivyo vinavyowasisimua mashabiki wake, na yeye analijua hilo na ndiyo maana ameamua kuyaishi maisha hayo.

Mtindo wake wa uandishi ni wa matukio ya kustaajabisha tu, na hata majina ya vitabu vyake ni ya kufikirika kutoka kuzimu.

Anaandika vitabu vinavyotathmini matukio ya kiasili ambayo yeye hayaamini kabisa. Ila si kila mtu anacho akipendacho na ndiyo maana mashabiki wake wanamnyima usingizi kutaka kuonana naye, waandishi wa habari wanatamani sana kujua siri ya mafanikio ya vitabu vyake na heshima inaongezeka mara dufu huku jina lake likizidi kukua. Huyu si mwingine, ni mwandishi mahiri wa hadithi ya ‘Ten Nights in Ten Haunted Houses’.

Anaitwa Michael “Mike” Enslin, ambaye ameachana na mkewe Lily baada ya kifo cha binti yao Katie. Baada ya kitabu chake cha hivi karibuni, Mike anapokea kadi ya posta inayotoka kwa mtu asiyejulikana ikionesha picha ya The Dolphin, hoteli iliyoko eneo la Lexington Avenue jijini New York. Kadi hii ina ujumbe usemao: “Usiingie katika chumba namba 1408.”

Inasemekana kuwa hicho ni chumba cha ajabu na watu hawakitumii kabisa kwa sababu hiyo. Mike anaiona hii kama changamoto, na anaamua kufunga safari kwenda katika hoteli ya The Dolphin, ili apatiwe chumba namba 1408.

Kumbuka huyu ni mwandishi anayependa kufanya uchunguzi wa jambo lolote kabla ya kuliandika, ni mtu asiyeamini katika uchawi wala mizimu japo vitabu vyake vinahusu mambo hayo, na sasa anataka kujua siri ya chumba hicho ndani ya hotel ya The Dolphin.

Anafika na kuingia hotelini na anaomba apatiwe chumba anachokihitaji lakini anakataliwa, anapouliza kama yeye hajulikani pale anajibiwa kuwa “wewe ni mtu maarufu sana ila hiki chumba hakikujui.” Meneja wa hoteli hiyo, Gerald Olin, anajaribu kumkatisha tamaa.

Anamwelezea Mike kuwa katika miaka 95 iliyopita, hakuna mtu aliyechukua zaidi ya saa moja ndani ya chumba namba 1408; na takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa kumekuwepo na vifo 56. Pamoja na Meneja wa hoteli hiyo kujaribu kumzuia Mike na hata kumhonga ili asiingie katika chumba hicho, lakini Mike anasisitiza kutaka apewe chumba hicho na maandalizi yafanywe bila kusita.

Anamwambia Meneja wa hoteli hiyo kuwa anataka kuandika kitabu ambacho hata wao watakipenda na kinatokana na yale aliyoyasoma yanayokihusu chumba hicho. Anaonywa tena na tena lakini hataki kusikia chochote. Anaandaa jina la kitabu chake kipya na anapania kuyaishi mazingira ya kitabu chake hapo hotelini ndani ya chumba namba 1408.

Hakika asiyesikia la mkuu huvunjika guu. Hakujua! Anaruhusiwa kuingia ndani ya chumba namba 1408 kutokana na umaarufu wake ili aweze kutimiza lengo lake la kuandika kitabu alichokusudia.

Pasipo kujua, mwandishi huyu mahiri anakialika kifo chake mwenyewe, milango ya chumba hiki inamruhusu kuingia ndani lakini si kutoka. Yanapomkuta analia sana kwa kuwa sasa kitabu kinamponza. Anaamua kukubaliana na ukweli na kujuta kwa kuweka umaarufu mbele na kutowasikiliza wengine.

Waswahili wanasema; ‘majuto ni mjukuu’! Je, unataka kujua kama mwandishi huyu alifanikisha azma yake ya kuandika kitabu na kutoka hai? Itafute filamu hii ya 1408 uitazame, hakika utagundua kuwa waandishi wa vitabu wanapitia mengi magumu, hasa wale waandishi ambao wanapenda kufanya uchunguzi kabla ya kuandika.

Lakini si lazima uiangalie filamu hii kama unahisi una ugonjwa wa woga. 1408 ni filamu ya Hollywood yenye kisa cha kutisha iliyotoka mwaka 2007, imetokana na hadithi fupi ya Stephen King ya mwaka 1999 yenye jina hilo hilo la ‘1408’. Filamu hii imeongozwa na Mikael Håfström na imewashirikisha nyota wa filamu za Hollywood kama John Cusack na Samuel L. Jackson.

Ilitolewa rasmi Juni 22, 2007 nchini Marekani, ingawa Julai 13 inatajwa kama tarehe rasmi ya kutolewa kwenye wavuti. Mapokezi Kwenye mtandao wa wahakiki na wakosoaji wa filamu wa Rotten Tomatoes, filamu hii imepewa asilimia 80, hii ni kulingana na maoni toka kwa wahakiki 176, na wastani wa alama 6.66 kati ya 10.

Kwenye mtandao mwingine wa wahakiki wa filamu wa Metacritic, filamu hii imepewa wastani wa alama 64 kati ya 100, kulingana na maoni ya wahakiki 27. Katika wiki yake ya kwanza ya ufunguzi, filamu hii ilifanikiwa kuingiza kiasi cha Dola za Marekani milioni 20.6 zilizotokana na maonesho ya sinema kwenye majumba 2,678.

Filamu hii imetengenezwa kwa bajeti ya Dola za Marekani milioni 25, na imeweza kuingiza jumla ya Dola za Marekani milioni 132, kati ya hizo Dola za Marekani milioni 71.9 zimetoka katika nchi za Canada na Marekani.

Habari Zifananazo

5 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button