Visa vya kichaa cha Mbwa vya pungua Singida
VISA vya ugonjwa wa kichaa cha mbwa katika Mkoa wa Singida vimepungua kutoka asilimia 30 mpaka kufikia visa viwili kwa kila mwezi.
Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na Ustawi wa Wanyama Nchini (EAAW) limesema hatua hizo zimetokana na juhudi zinazofanywa na serikali pamoja na wadau wengine kwa kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa Mkoani humu.
Mkurungenzi Mtendaji wa Shirika hilo Ayubu Nnko amesema shirika hilo pekee wamekuwa wakishirikiana na serikali toka mwaka 2018 ambapo wametoa chanjo kwa mbwa 5202 toka mwaka 2019 mpaka 2022.
“Shirika la EAAW na sisi hatuakuwa nyuma katika kiunga serikali mkono katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa mbali na kuwa sehemu ya shughuli zao pia tumekuwa tunatoa chanjo kwa mbwa dhidi ya ugonjwa huo,” amesema.
Katika kuadhimisha siku ya kichaa cha mbwa duniani Septemba 28 mwaka huu, Shirika hilo pia lilitoa chanjo kwa mbwa 518 na paka 29 katika Wilaya ya Mkalama Mkoani Singida.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) maambukizi ya kichaa Cha mbwa husababisha vifo vya makumi ya maelefu ya watu kila mwaka hususani Asia na Afrika.
Shirika hilo linasema asilimia 40 ya watu wanaong’atwa na wanyama wanaosambaza ugonjwa huo wakiwemo mbwa ni watoto wenye umri chini ya miaka 15.
Ugonjwa huo unasababishwa na virusi aina ya Rabies ingawa una chanjo bado unapatikana katika nchi na maeneo zaidi ya 150 duniani.