Vita Urusi na Ukraine yaathiri biashara ya madini

WIZARA ya Madini imelieleza Bunge kuwa vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine imeathiri biashara ya madini duniani.
Waziri wa Madini, Dk Doto Biteko amesema vita hiyo imesababisha ongezeko la mahitaji baadhi ya madini ikiwamo dhahabu, palladium, nickel, aluminium, cobalt na madini ya kinywe na bei ya dhahabu imeongezeka.
Dk Biteko amesema hayo bungeni Dodoma wakati anawasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Alisema uchumi wa madini nchini kwa kiasi kikubwa unatokana na madini ya dhahabu ambayo huchangia takribani asilimia 80 ya mapato yatokanayo na rasilimali madini.
Dk Biteko alisema katika kipindi cha kuanzia Julai mwaka jana bei ya dhahabu kwa wakia ilipanda kutoka Dola za Marekani 1,736.4 hadi kufikia Dola za Marekani 1,854.5 Machi mwaka huu.
Alisema kuongezeka kwa bei ya dhahabu kunatokana na sababu mbalimbali yakiwamo mahitaji ya madini hayo duniani.
“Kumekuwa na ongezeko la mahitaji ya baadhi ya madini ikiwemo dhahabu, palladium, nickel, aluminium, cobalt na madini ya kinywe, ongezeko hili limetokana na sababu mbalimbali ikiwemo vita kati ya Urusi na Ukraine,” alisema Dk Biteko.
Alisema hali hiyo imetokana na baadhi ya madini hayo yanayozalishwa na Urusi kuwekewa vikwazo kuingia kwenye masoko ya dunia hivyo kutengeneza fursa ya uhitaji kwenye nchi nyingine zinazozalisha madini hayo ikiwamo Tanzania.
Aliwaeleza wabunge kuwa bei ya madini ya almasi ilipungua katika soko hilo kutoka Dola za Marekani 296.63 kwa karati hadi kufikia Dola za Marekani 265.78 kwa karati katika kipindi cha mwezi Julai mwaka jana hadi mwezi Machi mwaka huu.
Alisema kushuka kwa bei ya madini ya almasi kumetokana na kupungua kwa uhitaji wa madini hayo kulikosababishwa na mtikisiko wa kiuchumi hususani katika nchi za Bara la Ulaya kutokana na athari za vita kati ya Urusi na Ukraine.
“Wizara inachukua hatua mbalimbali katika kutafuta masoko mengine ya kimataifa ya almasi yenye bei nzuri kama nchi za Falme za Kiarabu ambazo zina uhitaji mkubwa wa almasi, kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji na kuangalia uwezekano wa kupunguzwa kwa baadhi ya kodi na tozo kwa wachimbaji ili kuwaongezea wigo wa faida na kuchochea uzalishaji zaidi,” alisema.
Aidha, alisema wizara itaendelea kuhimiza uwekezaji katika madini mkakati yakiwemo palladium, nikeli, aluminium, cobalt, lithium na kinywe ili kunufaika na ongezeko la mahitaji ya madini hayo duniani.
Mining Census 2023
Watanzania mnakaribishwa kwenye SENSA ya Madini 2023 yenye lengo la kujua idadi ya migodi Tanzania, Idadi ya wachimbaji au watanzania wanaoshughulika na sekta ya Madini, Hali ya uchimbaji wa madini (zana zitumikazo kwa kila mgodi, aina ya teknolojia) na mapendekezo ya mbinu za kuboresha Sekta ya Madini.