Kizimkazi ni kijiji kilichopo katika Kata ya Kizimkazi Mkunguni, takribani 56 kutoka Mjini Unguja, Zanzibar. Wenyeji wa eneo hili, lenye wakazi 2,617, wamejikita katika shughuli za kilimo.
Utajuaje umefika Kizimkazi? Nyumba za wenyeji ambao ni Waswahili zimeezekwa kwa makuti. Uzio unaosaidia kuleta faragha nyumbani nap engine kuzuia vumbi na adha nyinginezo ni wa makuti vilevile. Kizimkazi ni eneo linalotajwa kuwa halijaathiriwa sana na utalii katika Visiwa hivyo.
Huku ukiwa umepata picha eneo hilo, unachopaswa kutambua kuwa wenyeji wa eneo hilo ni Waswahili wa Unguja pekee japo unaweza kupigwa na butwaa kukutana na raia wa kigeni wanaojichanganya na wenyeji katika harakati za kimaisha. Iwe Kizimkazi au Paje, usishangae kukutana na wenyeji wanotambuliwa na wenyeji Waswahili kama ‘wazungu’.
Naam, hawa ni raia wa Ukraine, ambao wameyakubali maisha ya wenyeji na sasa ni sehemu ya Waswahili wenyewe. Kama unatokea Bara au sehemu nyingine za visiwani, usishangae ukipokelewa na ‘mzungu’ huku akikukaribisha kufurahia mazingira mwanana na ya asili huko Kizimkazi.
Vladyslava Yanchenko, 27, ni mwanamke mwenye taaluma ya masoko. Akiwa pamoja na kaka yake aitwaye Viktor Tkachov (45), raia hao wa Ukraine waliwasili Zanzibar kwa ajili ya kujionea maajabu na uzuri wa eneo hilo zaidi ya mwaka mmoja uliopita. Hakika walipata jambo la kusimulia mara tu warudipo nyumbani kwao lakini hadi sasa hawajaweza kufanya hivyo kutokana na vita vinavyoendelea hivi sasa baina ya Urusi na Ukraine.
Ilikuwa ni changamoto kwa ndugu hao ya kurudi nyumbani hivyo kulazimika kuendelea kubaki Zanzibar baada ya kukata kiu yao ya utalii. Kwao ilikuwa changamoto kubwa zaidi. Ukaribu na mapenzi ya wenyeji wao yaliwateka, ghafla wakazoea maisha na sasa ukiendea eneo la Kizimkazi, usishangae ukakaribishwa na raia hao wa Ukraine.
“Siku hiyo ni ya kumbukumbu kubwa kwangu. Ilikuwa Februari 24, 2022, majira ya saa 11 asubuhi, hali ilibadilika katika nchi yangu (Ukraine), tulipata taarifa ya kuwepo kwa sauti za risasi na mabomu huku watu wakikimbia huku na kule kwa lengo la kujificha, ikiwa bado hawakufahamu nini kiliikumba nchi yangu,” anasema Vladyslava.
Vladyslava na raia wengine wa Ukraine walifahamishwa kwamba baadae walifahamishwa kwamba nchi yao imetumbukia katika vita, jambo ambalo binafsi lilimuumiza na kumpa hofu juu ya usalama wa ndugu zake ambao alikuwa amewaacha nyumbani kwao. Kingine ni kuwa matumaini ya kurudi Ukraine na kuendelea na kazi yake kama afisa masoko yalififia.
Hata hivyo, alijifunza ya kwamba kuwa mwanamke katika hali kama hiyo ni jasiri ambaye majukumu makubwa ni kujilinda, kuwalinda wengine na kuongoza jamii inayomzunguka kwa ujumla wake.
Pamoja na hilo, haikuwa rahisi kushuhudia picha za ndugu zake zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii na kuonyeshwa kwenye luninga namna wanavyokimbia kutafuta msaada wa kujificha. Ni hali iliyomtesa kisaikolojia.
“Nilipata taarifa kwamba huko nyumbani wanawake na mabinti wanabakwa na maaskari huku wodi za wajawazito na watoto zikichomwa moto bila huruma na kupoteza taifa lijalo,” anasimulia Vladyslava.
Vladyslava anaeleza kwamba nchini kwao, watoto walitambua umuhimu wa kujilinda, wakaelewa kuwa walihitaji ujuzi wa kulinda afya yao ya kimwili na kisaikolojia. Hamu ya kujifunza na kukua ikawa mwanga wa tumaini katika kipindi hiki kigumu kwao.
Maisha mapya, ndugu wengine
“Athari za vita zilisambaa katika mataifa yote na maisha yetu yakabadilika kabisa. Lakini katikati ya fujo na kutokuwa na matumaini, nuru ikaangaza tena. Leo, ningependa kushiriki nanyi katika mtazamo wangu juu ya jinsi ya kuwa mwanamke kutoka Ukraine kumebadili maisha yangu na kunipa uwezo wa kukumbatia mabadiliko na kusonga mbele kwa nguvu isiyoyumba kama wanaume,” anasema raia huyo wa Ukraine.
Kutokana na mapito hayo, raia huyo anasema kuna umuhimu wa kuwa na uwezo wa kujitegemea na kuliinda nafsi yake katika hali yoyote ile. Ili kufanikisha hilo, kujiandaa kimwili na kifikra lilikuwa ni suala la msingi, pengine kuliko mengine. Hali hii ilimfanya kukabiliana na changamoto mbalimbali za kimaisha ikiwa ni pamoja na kukubali kuishi maisha mapya.
“Nilifika nchini Tanzania kama mtalii, mahali ambapo ninaishi kwa sasa. Nimegundua dunia tofauti. Hapa, wanawake wanafanikiwa na kustawi. Ni mahali ambapo wanawake na wanaume wanaishi kwa umoja, wakisaidiana na kusaidia wengine,” anasema Vladyslava.
Vladyslava anaeleza kwamba Kizimkazi, Unguja Zanzibar ni mahali anapoishi kwa sasa na kupafurahia kwa kutaja sifa zake. Anasema wanawake hawakubali kufungiwa ndani bali wanapokea changamoto na wanakamiliana nazo. Wanapambana kwa ajili ya maendeleo, kusaidiana na kujenga mustakabali wao wa kesho.
Anasema kuwa yeye na kaka yake wapo tayari kuanzisha familia Unguja, shukrani kwa upendo, amani na utulivu visiwani humo.
“Mungu ibariki Tanzania, Tanzania Kwanza,” anamalizia Vladyslava.
Comments are closed.