Vitambulisho vya NIDA sasa mtandaoni
MSONGAMANO wa watu katika ofisi mbalimbali za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) wakati wa usajili na muda mwingi unaotumika kukamilisha usajili kwa mfumo wa sasa, ni miongoni mwa mambo yaliyosababisha kubuniwa na kuzinduliwa kwa mfumo mpya wa usajili wa vitambulisho kwa njia ya mtandao.
Uzinduzi wa mfumo mpya utasaidia kuongeza ufanisi wa utoaji wa vitambulisho pamoja na kuongeza idadi ya waombaji wa vitambulisho.
Hiyo inatokana na kazi hiyo kurahisishwa na sio lazima watu wasafiri kwenda ofisi za NIDA badala yake kila mtu anaweza kutumia ama simu janja au kompyuta mpakato kuingiza taarifa zake sahihi mahali husika.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha mamlaka hiyo, Geoffrey Tengeneza aliwaambia waandishi wa habari jana Dar es Salaam kuwa wakati mfumo mpya ukizinduliwa, mfumo wa zamani utaendelea kutumiwa.
Tengeneza alisema kwa sababu sio kila Mtanzania anamiliki simu janja na kinachotakiwa kufanywa kwa mwombaji ni kuingia kwenye mtandao wa intaneti kupitia online.nida.go.tz na kufuata maelekezo.
Alisema NIDA imeamua kupeleka huduma mikononi mwa watu ili kuepusha makosa mbalimbali yaliyokuwa yakijitokeza kama ya kukosea majina ya watu wakati wa kumsikiliza mwombaji pamoja na kukosea miaka ya kuzaliwa, lakini sasa mwombaji atakuwa katika hali ya utulivu nyumbani na kujaza fomu kwa mtandao kwa utulivu na kuepusha makosa kwenye utoaji wa taarifa.
“Faida za matumizi ya mfumo huu ni pamoja na kuepuka msongamano na foleni ambavyo huleta usumbufu mkubwa kwa waombaji, kuokoa muda ambao mwombaji anaweza kuutumia kwa ajili ya uzalishaji katika shughuli zake badala ya kukaa foleni kuanzia asubuhi mpaka ofisi zinafungwa,” alisema Tengeneza.
Aliongeza kuwa mfumo huo unalenga kurahisisha usajili wa wageni pamoja na raia wakazi wakiwamo Watanzania wanaoishi nje ya nchi kwa kushirikiana na balozi za Tanzania katika baadhi ya nchi.
Alisema baada ya kukamilisha fomu, mwombaji atapaswa kuichapa na kuipeleka ofisi za serikali za mtaa anapoishi ambao wataijaza na kugonga mhuri sehemu yao.
Mwombaji atalazimika kuchukua barua ya utambulisho na kuijaza na kisha kuiwasilisha pamoja na fomu katika ofisi za NIDA zilizoko karibu naye.
Tengeneza alisema matarajio ya NIDA kutokana na mfumo huo ni kuongezeka idadi ya wananchi watakaosajiliwa, kuiwezesha NIDA kutoa huduma bora zaidi kwa kuwa wafanyakazi watakuwa na utulivu kutokana na kupungua au kuisha kabisa kwa msongamano.
Alisema kwa kutumia mfumo wa zamani, mpaka sasa NIDA imesajili watu milioni 23 na vitambulisho milioni 11.9 vimezalishwa kutokana na usajili huo; vitambulisho milioni tisa vikiwa vimegawiwa kwa wananchi na watu milioni 19.84 wakipata namba pekee za vitambulisho.
Wazo la kuanzisha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa kwa raia wa Tanzania na wageni waishio nchini lilizaliwa mwaka 1968, likatungiwa sheria mwaka 1986 na kuanza kufanyiwa kazi mwaka 2006 baada ya upembuzi yakinifu kufanyika.