Vitendo vya ukatili Geita vyapungua kwa 63%

VITENDO vya ukatili mkoani Geita kwa watoto, kina mama na wanaume vimeripotiwa kupungua kwa asilimia 63 kwa mujibu wa rekodi za kuanzia Oktoba mwaka jana hadi Machi mwaka huu.

Ofisa wa Shirika la Usimamizi na Maendeleo ya Afya (MDH), Benjamin Kadikilo amesema hayo mjini Geita na akasema takwimu hizo zimetolewa na dawati la jinsia.

Kadikilo aliwaeleza waandishi wa habari kuwa kwa mujibu wa rekodi za miezi mitatu kutoka Oktoba hadi Desemba mwaka jana yaliripotiwa matukio 5,290 huku kwa kipindi cha Januari hadi Machi, mwaka 2023 yameripotiwa matukio 3,333 pekee.

Alisema kwa robo ya mwisho ya mwaka jana kati ya matukio 5,290 yaliyoripotiwa, kati yake kesi 302 ni za matukio ya ukatili wa kingono huku ukatili wa kihisia na kimwili ni kesi 4,988.

Kadikilo alisema kwa robo ya kwanza ya mwaka huu matukio ya ukatili wa kihisia kama vile kupigwa, kutelekezwa na kutishwa ni matukio 3,095 huku matukio 238 ni kubakwa na kulawitiwa na kufanya jumla ya matukio hayo 3,333.

Alisema kupungua kwa matukio ya ukatili ni matokeo ya MDH kufanya mradi wa Faith and Community Initiative unaoshirikisha viongozi wa dini, walimu wa malezi, viongozi wa kijamii kupinga ukatili wa watoto miaka 9-14.

“Pia kupitia mradi wa Coaching Boys Into Men tumefikia watoto 1,500 wa kati ya miaka 9-14 kwenye shule 12 ndani ya wilaya ya Geita ambazo kiukweli tumeanza kuona mabadiliko makubwa,” alisema Kadikilo.

Aliongeza: “Matukio mengi sasa hivi hususani ubakaji yanafanywa na ndugu, kwa hiyo imekuwa na changamoto namna ya kuyaripoti, kuna sababu nyingi ikiwemo sababu ya kiuchumi aliyefanya pengine ndio mlezi wa familia.”

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button