VITUO 32 vilivyobainika kujihusisha na udanganyifu vimefungiwa kuhudumia wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), ikiwa ni mapambano dhidi ya udanganyifu wa kihuduma unaofanywa na baadhi ya vituo vya kutolea huduma za matibabu.
Hayo yamebainishwa katika taarifa za NHIF ambazo zimeeleza kuwa vituo hivyo vilichukuliwa hatua ya kusitishiwa mikataba ya kutoa huduma kutokana na kubainika kufanya vitendo vilivyolenga kuvinufaisha vituo hivyo na kuuhujumu Mfuko.
Taarifa hizo zimetaja kuwa makosa yaliyothibitika ni pamoja na kuwasilisha madai kwa huduma ambazo hazikutolewa kwa wanachama wa Mfuko, kuwasilisha madai ya huduma za gharama za juu tofauti na huduma halisi iliyotolewa, kudai ada ya kumwona daktari bingwa ili hali mgonjwa alionwa na daktari wa kawaida pamoja na kutunza kumbukumbu za uongo kwenye vituo vya huduma ili kuhalalisha madai ya uongo yaliyowasilishwa NHIF.
Mbali na hatua ya kuvifungia vituo hivyo, hatua zingine ni pamoja na taarifa ya uchunguzi kuwasilishwa kwenye Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) kwa ajili ya hatua zaidi na vituo kuamriwa kurejesha kiasi cha fedha zilizobainika kuwa ni za udanganyifu.
“Vituo hivi 32 ambavyo vimesitishiwa mikataba kuanzia mwaka 2021 hadi sasa vimefanya udanganyifu wa jumla ya shilingi bilioni 2.5 ambazo Mfuko umewataka kuzirejesha na hatua zingine kuchukuliwa,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Akizungumzia uchunguzi unaofanywa na NHIF, Meneja wa Kitengo cha Kupambana na Udanganyifu, Dk Rose Ntundu alisema katika kipindi cha kuanzia Julai 2018 hadi Machi 2023, Mfuko ulifanikiwa kufanya jumla ya chunguzi za kina 556 ambazo zimefanikisha udhibiti na kurejesha fedha ndani ya Mfuko.