VITUO 26 vya kutolea huduma za afya mkoani Pwani vimefungiwa.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Gunini Kamba alisema hayo mjini Kibaha wakati akifunga kikao cha wadau wa vituo vya afya binafsi, timu ya usimamizi wa huduma za afya mkoa na msajili hospitali binafsi.
Kamba alisema vituo 133 vya watoa huduma binafsi vilikaguliwa na vilipewa maelekezo kutokana na upungufu uliokutwa.
Alisema vituo tisa vilikutwa havina usajili kabisa (vituo bubu) lakini vinatoa huduma jambo ambalo ni kosa kisheria.
Kamba alisema baadhi vituo hivyo vilitumika kwa kliniki zilizolaza wagonjwa wakiwamo wajawazito waliokwenda kujifungua.
“Baadhi ya vituo hivyo vya afya vilikutwa na upungufu vingine vilikutwa na mhudumu mmoja ambapo wahudumu wa afya hawaruhusiwi kutibu wagonjwa bali kuhudumia na kufanya usafi.
“Vitu vingine ambavyo vilikuwa na makosa makubwa vilichukuliwa hatua za kisheria na vile ambavyo vilikutwa na upungufu mdogo mdogo vilitakiwa kuurekebisha ili waendelee na utoaji huduma,” alisema.
Aidha, alisema baadhi ya vituo upungufu wao umetokana na watumishi kuacha kazi baada ya kupata ajira serikalini hivyo kuwa na upungufu na hawakujaza nafadi hizo.
“Vituo hivyo vinapaswa kuwapatia mafunzo watumishi wapya ambapo hata wao huwapatia mafunzo hasa wale wa ajira mpya ili waendane na taratibu za kazi kwani wanaisadia serikali katika kuwahudumia wananchi,”alisema Kamba.
Dk Ester Mwentumba alisema baadhi ya vituo vimesajiliwa kwa ajili ya maabara lakini vinatibu na kulaza wagonjwa na vinatoa huduma za kiafya jambo ambalo ni kosa.
Mwentumba alisema maabara ikishapima wanatakiwa wampe majibu aende kwenye kituo kilichosajiliwa kwa ajili ya kutibu ili mgonjwa apate matibabu.
Mratibu wa Shughuli za Ubia Baina ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) Mkoa wa Pwani, Alfred Ngowi alisisitizi kusimamia sheria, kanuni na taratibu za miongozo ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
Ngowi alisema vituo hivyo vinapaswa vizingatie huduma bora hivyo lazima wazingatie taratibu zilizopo kwani serikali imetoa kanuni sheria na miongozo ya wao kutoa huduma.