DODOMA; Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema serikali ipo katika mpango wa kuongeza vituo vingine vinne vitakavyoweza kutoa huduma ya saratani kwa njia ya mionzi.
Akijibu swali bungeni mjini Dodoma, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema vituo hivyo vitajengwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Aga Khan, KCMC Moshi na hospitali nyingine itajengwa huko Zanzibar.
kwa sasa hospitali ambazo zinatoa huduma hiyo ni Hospitali ya Kanda ya Bugando, Hospitali binafsi Besta, Hospitali ya Samitarian St. Francis iliyoko Ifakara na Ocean Road iliyoko jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo Waziri Ummy amesema serikali itaendelea kuwahamasisha wananchi kupima visababishi vya ugonjwa wa saratani ambavyo vipimo vyake ni salama.
“Chanjo hii ni salama haihusiani na kushindwa kupata ujauzito, ama masuala ya uzazi wa mpango chanjo hii ni salama na inawakinga wasichana kupanga saratani ya shingo ya kizazi,”amesema Waziri Ummy.
Amesema kutokana na ongezeko kubwa la mahitaji ya wagonjwa wa saratani, serikali imepanga kuangalia namna ya kuboresha huduma za bima ya afya ili kuhakikisha kila mtanzania mwenye ugonjwa apatiwe huduma kwa uhakika na kupunguza gharama kwa wagonjwa.