Vituo vya kisasa vya ukaguzi wa magari kujengwa mipakani

ARUSHA: Katika kuhakikisha ajali za Barabarani zinapungua kama sio kuisha kabisa, jeshi la polisi kwa kushirikiana na Shirika la Viwango Nchini (TBS) litajenga vituo maalumu vya ukaguzi wa magari maeneo yote ya mipakani ambapo itafungwa mitambo ya kisasa kwa ajili ya ukaguzi huo.

Hayo yamesemwa leo na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Nchini, Naibu Kamishna wa Polisi DCP Ramadhan Ng’anzi wakati alipofika katika Wilaya ya Longido mkoani Arusha kwa ajili ya kukagua eneo ambalo limetolewa na Wakala wa Barabara (TANROAD) ambako kituo hicho kitajengwa kwa Mkoa wa Arusha.

Kamanda Ng’anzi amebainisha kuwa vituo hivyo vitatumika kukagua magari yote ambayo yanaingia Nchini toka nchi jirani kwa ajili ya kukagua ubora wa magari hayo ambapo yale mabovu hayataruhusiwa kuingia hadi yatakapotengenezwa.

Advertisement

Aidha amewataka wamiliki wa vyombo vya moto kuhakikisha wanatimiza wajibu wa kisheria wa kukagua vyombo vyao kama inavyoelekezwa katika sheria kwani jeshi la polisi halitakuwa na muhali kwa wale watakaoshindwa kutii sheria bila shuruti.

Katika hatua nyingine Kamanda Ng’anzi amesema vituo hivyo pia vitajengwa maeneo yote ya mijini ambapo vitatumika kukagua magari yote yaliyopo nchini kama ilivyozoeleka kupitia wiki ya Nenda kwa Usalama ambapo wamiliki wa vyombo vya moto hupeleka vyombo vyao Ofisi za Usalama barabarani kwa ajili ya kukaguliwa.

Kwa upande wake Meneja wa TBS Kanda ya Kaskazini Mhandisi Joseph Mwaipaja amesema ameridhishwa na eneo hilo mara baada ya ukaguzi, hivyo Shirika hilo litaleta mitambo hiyo haraka iwekenavyo katika eneo hilo kwa ajili ya kufungwa ili kudhibiti ajali za barabani.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa TANROAD Mkoa wa Arusha Mhandisi Chilumba Mohamed amebainisha kuwa pindi kituo hicho kitakapokamilika kitasaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti magari mabovu ambayo mara kwa mara yamekua yakiharibu barabara.