Vituo vya Polisi Dar sasa wazi saa 24

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, amesema kuwa kutokana matukio ya uhalifu,  kuanzia sasa kila kituo cha polisi kitafanya kazi saa 24, tofauti na awali ambapo ilikuwa vipo wazi kuanzia asubuhi hadi jioni pekee.

Ametoa agizo hilo leo, alipokutana na wakuu wote wa wilaya za Dar es Salaam, viongozi wa vikosi vya ulinzi na usalama, viongozi mbalimbali mkoani humo na wilaya zake.

“Polisi hawatolala, kuanzia mapolisi kata, vikosi vya ulinzi shirikishi, mgambo wa jiji na polisi yeyote yule, watazunguka mtaa kwa mtaa, kata kwa kata, Dar es Salaam nzima na tumepata magari mengine  na askari 300 wameongezwa na kila kata kutakuwa na gari ya doria.

“Lengo ni kuongeza ulinzi na usalama mchana na usiku,” alisema Mkuu wa mkoa.

Septemba 15 mwaka huu alipozungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Zingiziwa, Chanika Wilaya ya Ilala, alitangaza operesheni ya nguvu itakayofanyika kutokomeza matukio ya uhalifu jijini Dar es Salaam.

“Watuhumiwa 125 katika matukio ya uhalifu yaliyofanyika Tabata, Kawe, Mizumuni na sehemu nyingine wamekamatwa wakiwemo wanunuzi 6 wakubwa wa vifaa vya wizi na kama mlivyosikia jana, wengine waliuawa katika harakati za kupambana na polisi walipokuwa wakielekea kutekeleza tukio jingine Makongo, ” alieleza.

“Watuhumiwa wengi ni kuanzia miaka 14-30 na wengi wao ni wale waliotoka Magerezani na kumaliza vifungo, hivyo wanarudi mtaani na kujiunga na vikundi vya uhalifu.

“Kuanzia leo, watuhumiwa wote wa uhalifu wakitoka gerezani, taarifa zao zitakuwa zinafuatiliwa kujua wako wapi na wanafanya nini,” amesema.

Pia amesisitiza jeshi la polisi na vikosi vya ulinzi shirikishi kuendelea na operesheni kwa wale wanaouza dawa za kulevya.

“Kwa kawaida huwezi kumkata mtu panga. Tumejiridhisha wahalifu wanatumia dawa za kulevya katika kutekeleza uhalifu na tulikamata kilo 63 za dawa za kulevya,” alisema.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema polisi watapambana usiku na mchana kuhakikisha wanarejesha amani.

“Jeshi la polisi hatujawahi kushindwa, tutapambana mchana na usiku kuhakikisha tunarejesha amani, watu wote wanaosaidia kusafirisha wahalifu, wanaonunua bidhaa za wizi, wanaofanya uhalifu na wanaoishi na wahalifu mtaani bila kutoa taarifa watakamatwa. Tujikite kuzuia uhalifu, kabla ya kupambana na wahalifu, ” alisema Kamanda Muliro.

Habari Zifananazo

Back to top button