VITUO vyote chakavu vya polisi vimefanyiwa tathmini na fedha zikishapatikana vitafanyiwa ukarabati wakati kipaumbele cha serikali sasa ni kujenga vituo katika maeneo yasiyokuwa na vituo.
Hayo yalielezwa Jumanne bungeni na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Jumanne Sagini wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Bupe Mwakang’ata (CCM).
Mbunge huyo alitaka kufahamu lini serikali itakamilisha ujenzi wa kituo cha polisi Sumbawanga.
Akijibu swali hilo, Sagini alisema kipaumbele cha serikali ilikuwa kuanza ujenzi wa vituo vya polisi katika maeneo ambayo hayakuwa na vituo vya polisi kabisa.
Sagini alisema kwa upande wa vituo chakavu tayari vimefanyiwa tathmini na kuwa wanasubiri fedha zitakapopatikana vitafanyiwa ukarabati unaostahili.
Kuhusu kituo cha polisi Sumbawanga, Sagini alimhakikishia mbunge huyo kuwa kwa sababu kituo hicho kipo karibu na mpakani na maeneo yenye matukio ya uhalifu, fedha zitakapopatikana kituo hicho ni moja ya vituo vitakavyopewa kipaumbele.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalumu, Jane Ntate aliuliza ni lini serikali itamaliza ujenzi wa kituo cha polisi Mbande Kata ya Chamazi.
Akijibu swali hilo, Sagini alisema kituo cha polisi Mbande ambacho ni cha Daraja B kilianza kujengwa kwa kutumia Sh milioni 16 zilizochangwa na wananchi Agosti mwaka 2016.
Sagini alisema kwa kutumia Sh milioni 38 zilizochangwa na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, mradi wa Songas na Kampuni ya Tatu Mzuka ujenzi uliendelea hadi upauaji mwaka 2020.
Alisema serikali kupitia Jeshi la Polisi ilitoa Sh 30,826,500 Juni 2022 ili kuendeleza na kukamilisha ujenzi huo kabla ya Novemba mwaka huu.