‘Viwanda vidogo 500 vya Wachina vimewekezwa Tanzania’

ZAIDI ya viwanda vidogo vidogo 500 vya Wachina vimewekezwa Tanzania ambavyo vimewezesha Watanzania wengi kupata ajira.

Hayo yamebainika wakati Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Pendo Malangwa alipofungua mashindano ya awali ya Siku ya Kichina Duniani yaliyoadhimishwa chuoni hapo.

Profesa Malangwa amesema asilimia kubwa ya Watanzania walioajiriwa katika viwanda hivyo ni wale wanaojua lugha ya kichina kupitia elimu inayotewa na Taasisi ya Confucius iliyopo chuoni hapo.

Amesema kupitia viwanda hivyo Watanzania wanaojifunza lugha ya Kichina wanaweza kuajirika katika viwanda hivyo.

Amesema Wachina wana mchango mkubwa katika kuunganisha nchi za kiafrika na China kupitia taasisi yake ya Confucius ambayo kazi yake kubwa ni kufundisha lugha ya kichina, utamaduni wake na michezo mbalimbali inayoendana na utamaduni wa Kichina.

“Ninashukuru Confucius kwa kuvuta wanafunzi kujifunza lugha ya kichina katika mazingira ya kiafrika.

“Lakini wamejifunza utamaduni wa kichina na kuutenda katika mazingira halisi, ni moja ya mahusiano ukijua lugha ya mtu unahusiana vizuri,” amesema.

Pia amesema kwa njia hiyo ya taasisi hiyo wameanza kuwaandaa walimu watakaofundisha kichina katika shule mbalimbali za Tanzania.

Naye Mhadhiri wa taasisi hiyo chuoni hapo Sharifu Matumbi, amesema wanaadhimisha miaka 13 ya kichina kwa kuwa ni miongoni mwa lugha kubwa duniani kwa wanafunzi kuonesha vipaji vyao mbalimbali kupitia lugha hiyo.

Amesema wanatumia njia mbalimbali kufundisha lugha hiyo ili wanafunzi waipende na kuielewa kwa haraka, wasome kwa bidi mwisho wa siku wapate ajira zitakazowawezesha kuwasiliana na Wachina.

Baadhi ya washiriki waliohudhuria maadhimisho ya siku ya kichina duniani.

Kwa upande wake mwanafunzi kutoka Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Evina Deogratius amesema anaisoma lugha hiyo kama lugha ya ziada kwa kuwa anachukua kozi ya masoko chuoni hapo.

“Ninapenda kujifunza lugha mbalimbali kikiwemo kichina kwa sababu kuna fursa nyingi ikiwemo kupata ajira,” amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa taasisi hiyo ya kichina UDSM, Profesa Xiaozhen Zhang amesema wanafunzi 29 wamesheherekea siku hiyo kwa kuonesha vipaji mbalimbali.

Awali amesema siku hiyo ya lugha za kichina ilizinduliwa na kitengo cha umoja wa mataifa cha mawasiliano mwaka 2010, lengo likiwa ni kukuza matumizi sawa katika lugha kubwa sita katika umoja wa mataifa.

 

Habari Zifananazo

Back to top button