Katika kuhakikisha upatikanaji wa dawa pamoja na vifaa tiba vinapatikana kwa wingi na kwa gharama nafuu, serikali imekamilisha ujenzi wa kiwanda cha barakoa pamoja na kuendelea na ujenzi wa viwanda vya bidhaa za afya.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Oktoba 17, 2022, Mkurugenzi Mkuu, Bohari ya Dawa (MSD), Mavera Tukai, amesema kuwa ujenzi wa viwanda hivyo uko katika hatua mbalimbali, huku akiikaribisha sekta binafsi kuendelea kuwekeza katika sekta ya afya.
Tukai amesema kuwa viwanda hivyo ni pamoja na kiwanda cha mipira ya mikono, vidonge, vimiminika na dawa za ngozi.
Ameongeza kuwa mpaka sasa kiwanda cha uzalishaji barakoa kimeshakamilika na kimeanza uzalishaji wa barakoa, kwa ajili ya watumishi katika sekta ya afya, pamoja na watumiaji wengine kama nyenzo ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya maradhi ya mfumo wa njia ya hewa hasa UVIKO-19.
Kukamilika kwa kiwanda hicho kimefanikisha kupunguza gharama za bei za barakoa na pia kuhakikisha vituo vya umma vya kutolea huduma vinakuwa na barakoa nyakati zote.