Viwanja 10,000 kupimwa wanaohamia Msomera

TANGA: Jumla ya viwanja 10,000 vinatarajiwa kupangwa na kupimwa katika sehemu ya eneo lililokuwa Pori Tengefu la Handeni awamu ya pili kwa ajili ya wakazi wanaohamia kutoka hifadhi ya  Ngorongoro.

Hayo yamebainishwa Machi 7 2024 na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi , Geophrey Pinda katika eneo linalotekelezwa  mradi wa kupima viwanja na mashamba wakati wa ziara ya pamoja ya Mawaziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na ile ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwenye eneo la Kijiji cha Msomera Handeni Mkoa wa Tanga.

Pinda amesema, kati ya viwanja hivyo viwanja 5000 ni kwa ajili ya makazi na 5000 ni mashamba. Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi viwanja 2500 vya makazi vitapimwa kwenye kijiji cha Msomera, viwanja 1500  kijiji cha Kitwai B (Simanjiro) na viwanja 1000 kijiji cha Sauyi (Kilindi).

Aidha, amesema hadi kufikia februari 28 mwaka huu jumla ya viwanja 5,882 vimepimwa sawa na asilimia 118 ya lengo la kupima viwanja 5000 katika maeneo ya upangaji yaliyopo vijiji vya Saunyi (Kilindi) na Msomera (Handeni).

Amebainisha kuwa, kati ya viwanja hivyo, viwanja 5,272 ni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za makazi pekee na hivyo kuwa na ziada ya viwanja 610 ikilinganishwa na malengo ya upatikanaji viwanja 5000.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button