Vunja Bei yaibuka ligi iliyomtoa Mzize

KAMPUNI ya Vunja Bei imeahidi kuifanya Ligi Daraja la Nne mjini Iringa, Ngajilo Municipal League kuwa bora na ya ushindani mkubwa kama moja ya mikakati yake ya kukuza vipaji na kuhakikisha Iringa wanapata timu itakayoshiriki Ligi Kuu

Ligi hiyo ngazi ya manispaa (wilaya) ndio chimbuko la mshambuliaji wa Yanga anayekuja juu, Waleed Mzize ambaye kabla ya kujiunga na timu hiyo alikipiga na timu ya Pentagon FC ya mjini Iringa pamoja na Tigers FC ya Ilula miaka mitano iliyopita.

Advertisement

Mkurugenzi wa masoko wa kampuni hiyo ambaye ligi hiyo itakayoshirikisha timu 10 msimu huu imepewa jina lake, Fadhili Ngajilo amesema; “Ni hasara kubwa kwa Mkoa wa Iringa wenye historia nzuri ya mpira wa miguu kutokuwa na timu ya Ligi Kuu.”

Ngajilo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa alisema kampuni yao itahakikisha ligi hiyo inatoa wachezaji wa kali watakaosaidia kuurudisha mkoa wa Iringa kwenye ligi kuu.

Akikabidhi vifaa vya michezo kwa timu 10 zitakazoshiriki ligi hiyo, Ngajilo aliwaalika wadau wengine wa mchezo huo kuiongezea nguvu ligi hiyo kwa kutoa ufadhili utakaoipa mafanikio zaidi.

“Pamoja na kuifadhili ligi hii, tunataka historia ya michezo Iringa itanuke zaidi na mwakani tuna mpango wa kufadhili mashindano ya ndodi, rede kwa wanawake na drafti,” alisema.

Viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Manispaa ya Iringa wameshukuru kwa ufadhili huo na wameomba wadau wengine wajitokeze kuinga mkono kampuni ya Vunja Bei katika kukuza mpira wa miguu mkoani Iringa.

Wakati huo huo Mkurugenzi wa Matukio Daima Media, Francis Godwin ameunga mkono juhudi za kampuni ya Vunja Bei kwa kuahidi kuongeza zawadi itakayotolewa kwa mshindi wa kwanza wa ligi hiyo.

Aidha Godwin ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa (IPC) amesema klabu hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa mchezo wa soka, watafanya kongamano kubwa litakalotumika kuchambua changamoto za maendeleo ya mchezo huo na kushauri namna ya kuzishughulikia.

3 comments

Comments are closed.