DODOMA: SERIKALI imesema msaada wa chakula ulioingizwa nchini ni salama kwa matumizi pia taratibu zote za uingizwaji na ukaguzi umefuatwa.
Taarifa iliyotolewa na Meneja Uhusiano na Masoko wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Gladness Kaseka imedadavua kuwa utaratibu wa kuongeza virutubishi kwenye chakula ‘food fortification’ unakubalika kitaalamu na hufanyika kwa lengo la kuboresha hali ya lishe kwa walaji.
“TBS itaendelea kusimamia kikamilifu jukumu la kuhakikisha kuwa chakula kinachoingia nchini kinakidhi vigezo vya usalama na ubora kwa mujibu wa matakwa ya viwango ili kuendelea kulinda afya za walaji,” imeeleza taarifa hiyo.
Siku kadhaa nyuma kuliibuka wasiwasi uliokuwa ukienea mitandaoni juu ya msaada wa chakula ukijumuisha (mchele ulioongezwa virutubishi, mafuta ya kupikia ya alizeti yaliyoongezwa virutubishi na maharage), ambao ulitolewa na Wizara ya Kilimo ya Marekani kwa ushirikiano na Taasisi ya Jumuiya za Kimataifa (Global communities) katika baadhi ya shule za mkoa wa Dodoma chini ya mpango uitwao ‘Pamoja Tuwalishe’.
TBS imewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwani suala la udhibiti wa usalama na ubora wa bidhaa ni mtambuka (shared responsibility).