VYAMA vya siasa Zanzibar vimefurahishwa na uamuzi wa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi wa kuongeza kiwango cha chini cha pensheni kwa asilimia 100 kwa wastaafu pamoja na wazee waliokuwa wakilipwa pensheni jamii.
Vimesema hatua hiyo inaonesha serikali inavyojali na kutambua mchango wao katika ujenzi wa taifa na ustawi wa jamii.
Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi ya Chama Cha Mapinduzi, Zanzibar, Mbeto Khamis Mbeto aliwaambia waandishi wa habari kuwa kitendo kilichofanywa na Rais Mwinyi ni kupokea na kutekeleza kilio cha muda mrefu cha wastaafu kuona kwamba na wao wanakumbukwa katika mabadiliko ya nyongeza za pensheni ili kwenda na wakati wa mabadiliko ya maisha.
Alisema kitendo cha kuongeza nyongeza ya pensheni kwa asilimia 100 kwa wafanyakazi wastaafu kinaonesha utu wa kutambua mchango wa watumishi hao ambao walilitumikia taifa lao kwa uadilifu.
”Chama Cha Mapinduzi Zanzibar kimefurahishwa na tamko la Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi la nyongeza kwa asilimia 100 kwa wastaafu ambao walikuwa wakipokea pensheni ya kiwango cha chini waliokuwa wakipokea shilingi 90,000 sasa watapata 180,000,” alisema.
Mwenyekiti wa Chama cha Ada Tadea, Juma Ali Khatib alisema hotuba ya Rais wa Zanzibar, Dk Mwinyi katika kilele cha Mei Mosi inaonesha mapenzi na hisani yake katika kuwajali watumishi wastaafu pamoja na kutambua mchango wao mkubwa kwa taifa na maendeleo.
Alisema yapo malalamiko ya siku nyingi kwa wafanyakazi wastaafu kupokea kiwango kidogo cha pensheni licha ya wengine kutumikia taifa muda mrefu katika maendeleo mbalimbali ya utumishi wao.
Alieleza kufurahishwa na uamuzi wa Rais Mwinyi wa kuongeza pensheni jamii kwa wazee waliofikisha umri wa miaka 70 ambao awali walikuwa wakilipwa Sh 20,000 na katika mabadiliko ya nyongeza sasa watalipwa Sh 50,000.
Mwakilishi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Kanda ya Afrika Mashariki, Maridadi Fanuel ambaye alihudhuria maadhimisho ya Mei Mosi Wilaya ya Kaskazini Unguja, alieleza kufurahishwa na ahadi nyingi zilizotolewa na Rais Mwinyi ikiwemo za kufanya kazi na shirikisho la vyama huru vya wafanyakazi katika kuona ufanisi wa kazi na uwajibikaji unafikiwa.
Mstaafu wa Idara maalumu ya kikosi cha KMKM, Zubeir Suleiman Ali alisema: “Suala la kuongezwa kwa pensheni kwa wafanyakazi wa kima cha chini lipo muda mrefu, tunamshukuru Dk Mwinyi amelisikia na kutangaza rasmi kuongeza nyongeza hiyo,” alisema.