KUELEKEA uchaguzi mkuu mwaka 2025 na uchaguzi wa serikali za mitaa, vyama vya siasa nchini vimetakiwa kuendelea kujadiliana na kusikilizana kwa hoja mbalimbali zitakazojenga vyama vyao pamoja na kupeana fursa ya kutoa maoni yatakayoboresha uendeshaji wa vyama na kukuza demokrasia nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Msajili wa vyama vya siasa Mohamed Ali Ahmed wakati akifunga mkutano wa kikao kazi wa viongozi wa vyama vya siasa nchini ulioanza Julai 17 na kumalizika leo Julai 18 uliolenga kutoa maoni juu ya uchaguzi na maandalizi ya kuelekea kwenye uhakiki wa vyama vya siasa.
Akizungumzia lengo la mkutano huo, Ahmed amesema ni kuendeleza safari ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwapa fursa watanzania ya kuzungumza na kutoa maoni waliyonayo ili kujenga tanzania yenye heshima na yenye watu wa kuheshimiana.
Ahmed amevitaka vyama vya siasa kutosita kutoa maoni waliyonayo huku akiahidi kuendelea kuyafanyia kazi maoni yote yaliyotolewa katika kikao kazi hicho.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba amesema bado ana wasiwasi mkubwa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa,vijiji na vitongozi kwasababu taratibu za kuufanya uchaguzi huo uwe wa haki na huru bado haujaandaliwa na hivyo kuisisitiza serikali kuandaa utaratibu huo.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT wazalendo, Bara Dorothy Semu amesema mkutano huo umewapa fursa nzuri ya kujua namna bora ya kuboresha chama pamoja na kutatua changamoto za chama katika utekelezaji wa majukumu yao.