WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu amezindua rasmi vyumba vipya vya kisasa sita vya mnyororo baridi vya kuhifadhia chanjo vilivyojengwa na Vodacom Tanzania kwa kiasi cha Sh miloni 600.
Kutokana na ujenzi wa vyumba hivyo Mpango wa Taifa wa chanjo sasa utakuwa na uwezo wa kutunza chanjo ujazo wa lita 130,000 kutoka ujazo wa awali wa lita 84,000.
Meneja wa Mpango wa Taifa wa Chanjo Dk Florian Tinunga, amesema awali walikuwa hawana vyumba vya kutosha kuhifadhi chanjo na walikuwa wanahifadhi bohari ya dawa (MSD), hivyo uwepo wa vyumba hivyo utafanya chanjo zote zihifadhiwe hapo.
Amesema hivi sasa kuna vyumba 16 vya kuhifadhi chanjo ambapo kwa nchi nzima mahitaji ni ujazo wa lita 120,000 hivyo chanjo zipo za kutosha.
Waziri Ummy amesema Msaada huo uliotolewa na Vodacom Foundation na Vodacom Group umekuja katika wakati ambao bara la Afrika linapitia changamoto za uhifadhi wa chanjo kwenye nchi mbalimbali.
“Utafiti uliofanywa na Shirika la Afya duniani (WHO), kanda ya Afrika kwenye nchi 34 za Afrika umebaini kuwa, katika asilimia 31 ya nchi hizo, zaidi ya asilimia 50 ya wilaya zake zina changamoto za usambazaji wa chanjo kutokana na ukosefu wa vifaa vya kuhifadhia madawa hayo,”amesema.
Ameeleza kuwa usimamizi wa mnyororo mzima wa vifaa baridi ni sehemu muhimu ya kuhakikisha usambazaji salama na mzuri wa chanjo na kwamba chanjo zinahitaji majokofu imara, ambayo yanakidhi mahitaji fulani ya joto, kutoka mahali pa utengenezaji hadi hatua ya mwisho ya usambazaji.
” Ikiwa mnyororo huu utavunjika wakati wowote inaweza kuathiri ufanisi mzima wa chanjo na kuzifanya zisiwe na uwezo za kuzuia maradhi,” amesema na kuongeza:
” Nawasihi watumishi wa sekta ya afya tu kuvilinda vifaa hivyo, lakini pia kutumia nafasi na ushawishi wetu kuhamasisha jamii kujitokeza kupata chanjo,” amesema Waziri Ummy.