Vyuo pamoja katika kubadilishana maarifa
DAR ES SALAAM: CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kinashirikiana na vyuo vingine katika kubadilishana maarifa, hivyo kudhamiria kuanzisha Kituo cha taaluma cha Bara la Asia hapa nchini.
Kaimu Naibu Makamu Mkuu chuoni hapo, anayeshughulikia utafiti, Profesa Nelson Boniface amesema hayo wakati wa majadiliano ya jinsi ya kuanzisha kituo cha taaluma kinachoitwa, ‘Africa Asia Studies’ chuoni hapo.
“Ukiwa na watafiti mbalimbali katika vyuo vikuu, ni kigezo kimoja wapo kitakachotumika kuangalia ninyi mnashirikiana na kina nani.
“Na katika ubadilishanaji wa maarifa ni kitu muhimu sana kwa sababu mkiwa mnajifungia ninyi kwa ninyi mtakuwa na maarifa ya pale pale .
“Ukiangalia sio kimataifa tu mpaka na mabara. Kwa hiyo tutarajie kwamba ni Afrika, Ulaya na Asia. Kwa hiyo ni kituo ambacho kinasaidia kumataifisha nchi zetu, pia kinahusiana na taaluma zetu ambazo zinatuhusu,”amesema.
Amesema kituo kama hicho cha taaluma kitakachoanzishwa, kipo sehemu nyingine kama Netherland, Thailand, Zambia na nyinginezo ambazo zimeshiriki katika majadiliano hayo.