KAGERA,Bukoba,Kamati ya kudumu ya Bunge ya Elimu,Utamaduni na michezo imetoa wito kwa wizara ya Elimu na Mafunzo ya ufundi kuhakikisha vyuo vya ufundi stadi VETA vilivyojengwa nchini vinakuwa na Karakana Bora za kisasa na Mafunzo yanajitosheleza ili kuwawezesha vijana wanahoitimu kujiajiri moja kwa moja wanapohitimu katika vyuo hivyo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Husna Sekiboko na wajumbe wa kamati walitembelea chuo Cha Mfano Cha Mafunzo ya ufundi VETA kilichopo mkoani Kagera na kuridhishwa na miundombinu mizuri ambayo imejengwa katika chuo hicho kilichogharimu Bilioni 22 ambapo walimwagiza Naibu waziri wa Elimu kuhakikisha chuo hicho kinakuwa na vifaa vyote vya Mafunzo vinavyohitajika.
Wajumbe wa kamati hiyo wamesema katika ziara ya kutembelea vyuo vya VETA nchini wamebaini upungufu mkubwa wa vitendea kazi vya kujifunzia licha ya serikali kuwekeza fedha nyingi katika ujenzi wa vyuo vya kisasa hivyo wanafunzi wengi wanajifinza kwa nadharia na kuwafanya kuona kila kitu kipya wanaporudi katika jamii kufanya kazi kwa vitendo.
“Kupitia kamati yetu tunapendekeza kuwa wizara ya Elimu chukueni hatua haraka za kuhakikisha ubora wa vyuo vilivyojengwa kwa fedha nyingi unaendana na Mafunzo ya vitendo yanayotolewa ili kujenga kizazi kinachoweza kujiajiri,kupunguza nafasi za watu wasiokuwa na ajira kwa sababu wanajamii wanataka watoto wao wakihitimu waje kuonyesha kile walichojifunza hivyo Kama mtoto hawezi kuwa na vifaa hawezi kuonyesha kile alichojifunza chuoni “amesema Sekiboko.
Maagizo mengine ya kamati ni kuhakikisha wizara ya Elimu inaajiri walimu wa kutosha katika vyuo vya ufundi ili kukidhi mahitaji na malengo ya serikali ya uwepo wa vyuo pamoja na kuhakikisha wanafunzi wa vyuo vya ufundi wanaofanya ubunifu kuunganishiwa moja kwa moja na soko la ajira kuliko kuwaacha wenyewe pale wanapohitimu.
Kwa mujibu wa Naibu waziri wa Elimu Sayansi na Tekinolojia Omary Kipanga amesema kuwa serikali imetenga kiasi Cha shilingi Bilioni 100 kuhakikisha vyuo 64 katika wilaya zote ambazo hazikuwa na vyuo vya ufundi Stadi na chuo kimoja katika mkoa wa Songwe ili kuhakikisha kila wilaya na mikoa yote Tanzania inakuwa na vyuo vya Ufundi Stadi VETA.
Amesema mpaka sasa serikali inaendelea kuwekeza katika vyuo vya ufundi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Karakana Bora,vifaa vya kufundishia pamoja na kutenga bajeti ya kuajiri walimu wenye uzoefu mkubwa watakaowezesha kuwafundisha vijana ili wakihitimu wakabiliane na ajira katika jamii zao.