Vyuo vyatakiwa kujenga ukaribu na wenye viwanda

VYUO Vikuu nchini vimetakiwa kujenga uhusiano na waajiri pamoja na wenye viwanda nchini, ili kuwezesha wahitimu wanapomaliza masomo yao waweze kupokelewa kwa ajili ya kupata ujuzi wa kufanya kazi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Carolyne Nombo amesema hayo wakati akishuhudia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kikiingia mkataba na taasisi mbili ambazo ni Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa), pamoja na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).

Profesa Nombo amesema makubaliano hayo yatawawezesha wahitimu wa chuo hicho kwenda kupata ujuzi katika maeneo hayo, kwa kuwa wanapotoka vyuoni wanaweza kuajiriwa ama kujiajiri wenyewe, hivyo wawe na mbinu za kukidhi mahitaji atakapokuwepo.

Advertisement

“Kumekuwa na changamoto kwa wahitimu ambao wanatoka kwenye vyuo vyetu wengi wana ujuzi, lakini ni ujuzi ambao hauwawezeshi kuingia kazini moja kwa moja.

“Kwa hiyo tukaona njia bora ya kuweza kuboresha eneo hilo ni kuwahakikisha kuwa vyuo vyetu vinakuwa na uhusiano na waajiri na viwanda, ambapo wahitimu wetu wanakwenda kufanya kazi. Kwa nini tuwe na uhusiano nao kwa sababu wao watatusaidia kujua mahitaji ya ujuzi ni yapi,” amesema.

Amesema pia waajiri kutoka sekta binafsi ama sekta za umma watasaidia kueleza mahitaji ya ujuzi unaotakiwa,  kutoa mawazo kwa ajili ya utafiti, kutoa fedha kwa ajili ya utafiti pia watasaidia wabunifu.

Amesema kupitia mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), unaotekelezwa na serikali katika vyuo vyake nchini, unahimiza wanafunzi kupata elimu ya vitendo ili kuondoa ile dhana kuwa wanaohitimu hawajaiva kuingia kwenye soko la ajira.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu kutoka TPSF, Raphael Maganga alisema wameingia mkataba wa makubaliano na UDSM, ili kukuza ujuzi wa Watanzania walio wengi hususan wanafunzi wanaohitimu kutoka vyuoni, ili wapate  ajira kwenye kampuni za sekta binafsi.

“Zaidi ya wanafunzi 100,000 mpaka milioni moja wanahitimu kila mwaka, kati ya hao unakuta chini ya asilimia 15 wanapata ajira rasmi, kwa hiyo  makubaliano haya ni kutatua changamoto ya jinsi gani kampuni za kitanzania zinaweza zikaajiri zaidi wahitimu wa vyuo vyetu.

“Lakni pia kampuni zetu ni jinsi gani zinaweza zikakuza ujuzi kwa wanafunzi, ili wakishahitimu wawe wanaajirika kirahisi na kuweza kufanya majukumu yao katika kukuza uchumi wa nchi,” amesema.

Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye, amesema lengo kubwa la kusaini makubaliano hayo ni kuzindua ushirikiano wa viwanda na vyuo vikuu kwa kuwa chuo hicho hakiwezi kwenda peke yake kinahitaji watu wa kuwashika mkono, ili kuhakikisha watoto wa Watanzania wanapata shughuli za kufanya.

Amesema kupitia mikataba hiyo UDSM itatoa ujuzi walio nao na kusaidia taasisi ambazo wamesaini nazo mikataba.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *