Waahidi kutunza misitu kuinua uchumi
MANYARA; Jamii ya Wahadzabe, Wadatoga na Masai kutoka Wilaya za Mbulu na Kiteto mkoani Manyara wamesema wataendelea kulinda na kutunza misitu ya asili kama njia mbadala ya kuinua uchumi wao.
Kauli hiyo imetokana na jamii hiyo kupata Sh bilioni 4 za biashara ya hewa ya ukaa ikiwa ni matokeo ya utunzaji wa misitu ya asili na mazingira.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Selemani Jaffo, alikabidhi mfano wa hundi ya Sh bilioni 4.
7 kutoka kwa kampuni ya Carbon Tanzania, ikiwa ni malipo ya fedha za uuzaji wa hewa ya ukaa iliyofanyika kwenye ukumbi wa Whiterose Babati.
Wanufaika hao wanatoka Vijiji vya Yaeda Chini na Makame vilivyopo Halmashauri za Wilaya ya Mbulu na Kiteto.
General Mathias, mnufaika kutoka jamii ya Wahadzabe alibainisha kuwa maisha ya Wahazabe, Wamasai na Wagatoga yanategemea misitu ya asili kwa ajili ya kurina asali na uwindaji.
“Tunaishukuru Kampuni ya Carbon kwa kuwa inalinda misitu ya asili na imetupa elimu ya kuacha kukata misitu hovyo na kuchoma moto kurina asali, kampuni ni rafiki wa kwetu pia,” amesema Mathias.
Waziri Jaffo amewaasa wananchi kuendelea kuiamini serikali yao kutokana na ahadi na mipango ya maendeleo inayotekeleza.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga alieleza kuwa fedha zilizotolewa zitasaidia kusomesha watoto kuanzia elimu ya msingi hadi vyuo vikuu na kujenga zahanati vituo vya afya na kurekebisha miundo mbinu ya Barabara.
NaYe Mkurugenzi wa fedha Kampuni ya Carbon Tanzania, Alphael Jackson aliwahakikishia wananchi hao kuendelea kutoa fedha ikiwa utunzaji wa mazingira utakuwa endelevu.