WAANDISHI wa habari 91 wameteuliwa kuwania Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari (EJAT) 2022, baada ya majaji tisa kupitia na kuchuja kazi 893 zilizowasilishwa. Kati ya wanahabari hao, wawili wanatoka Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) ambao ni Hazla Omar anayeandikia Daily News kutoka mkoani Arusha na Vicky Kimaro wa HabariLEO akiandika kutoka mkoani Dar es Salaam.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga alitangaza wateule hao jijini hapa katika mkutano wa waandishi wa habari na Mwenyekiti wa jopo la majaji, mwandishi mkongwe nchini, Mkumbwa Ally.
Mukajanga alisema idadi hiyo ya kazi 893 ni kubwa na pia idadi ya wateule haijawahi kuwa wengi kiasi hicho tangu kuanzishwa kwa tuzo.
Kwa mujibu wake, majaji hao saba walitumia siku tisa kufanya kazi hiyo Bagamoyo mkoani Pwani kuanzia Juni 10 hadi 18, mwaka huu.
Mwenyekiti wa jopo la majaji, Mkumbwa Ally alisema ongezeko la kazi nyingi linaonesha kuwapo kwa hamasa zaidi na kueleza kuwa ni kitu kinachopaswa kuendelea kila mwaka. “Kuna maboresho zaidi katika online (mitandao ya kijamii) ukilinganisha na kazi nyingine.
Zote ni perfect (nzuri), lakini kuna shida shida kidogo, kazi ni ndefu sana, online iwe fupi, iwe na picha, michoro,” alieleza Mkumbwa ambaye aliwahi kuwa Kaimu Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN). Majaji wengine ni Mwanzo Millinga, Peter Nyanje, Mbaraka Islam, Dk Egbert Mkoko, Rose Haji na Nasima Haji Chum.
Comments are closed.