Waandishi wa habari, asasi tegemeo kutokomeza ndoa za utotoni

Wakazi wa Wilaya ya Lindi wakitazama Filamu ya Ndoano katika utekelezaji wa mradi wa Sauti Zetu

KATIKA kupinga ndoa na mimba za utoto waandishi wa habari wana nafasi kubwa kuelimisha jamii kuhusu madhara ya ndoa hizo, ili kuwapa nafasi watoto wa kike kusoma na kutimiza ndoto zao.

Kwa mujibu wa sheria ya nchi mtoto ni yule ambaye ana miaka  0-18 ambapo katika kipindi hicho anakuwa chini ya uangalizi wa mzazi au mlezi.

Katika kipindi cha umri huo pia mtoto hataruhusiwa kufanya mambo mbalimbali ikiwemo kuajiriwa,kupiga kura, kupata leseni ya biashara , kupata leseni ya gari,k uingia mikataba na mambo mengine.

Advertisement

Hata hivyo wakati Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 inamtafsiri kuwa ni mtu yoyote mwenye miaka chini ya 18, Sheria ya Ndoa inaruhusu mtoto wa kike chini ya umri huo kuolewa.

Mwaka 2019, Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ilithibitisha uamuzi wa Mahakama Kuu katika kesi ya Rebeca Gyumi ya mwaka 2016 dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali kuwa vifungu vya 13 na 17 vya Sheria ya Ndoa vinavyoruhusu mtoto kuolewa kwa idhini ya wazazi akiwa na miaka 15 na mahakama akiwa na miaka 14 ni vya kibaguzi na ni kinyume na Katiba.

 

Mtoto aliyekumbana na mimba za utotoni akiwa amembeba mtoto

Katika uamuzi huo, Mahakama Kuu iliamua kuwa Sheria ya Ndoa ipitiwe upya, ili kuondoa ubaguzi na kukosekana kwa usawa kati ya umri wa chini wa ndoa kwa wavulana na wasichana.

Mahakama ilisema kuwa Kifungu cha 13 na 17 cha Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 kinakwenda  kinyume na Ibara ya 12, 13 na 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ambayo inatoa haki sawa kwa wote mbele ya sheria.

WAJIBU WA WAANDISHI WA HABARI

Marry Geofray ni mwandishi wa habari jijini Dar es Salaam, anasema ili kukomesha vitendo vya ndoa na mimba  za utotoni waandishi wa habari wana nafasi kubwa kuelimisha jamii madhara ya ndoa za utotoni.

“Kwa kiasi kikubwa vyombo vya habari kupitia waandishi wana nafasi kubwa katika kufanya mabadiliko na kutokomeza ndoa na mimba za utotoni kwa kutumia sauti zao na kalamu zao,”anaeleza Marry.

Mwandishi mwingine James Salvatory anasema waandishi  wa habari ni watu muhimu na wanaoaminiwa na jamii, hivyo taarifa wanazotoa zinaamini zaidi hivyo ni muhimu kuongeza ari ya kutoa elimu kwa jamii.

Anasema kupitia vipindi na makala mbalimbali katika Redio,TV ,Magazeti na mitandao ya kijamii waandishi wana ushawishi mkubwa kubadilisha fikra za wana jamii.

Watekelezaji wa mradi wa Sauti Zetu wakiwa na mtu wa matangazo kwa umma – Nyakitonto- Kasulu mkoani Kigoma.

“Unajua waandishi wana nguvu kubwa katika kubadili vitu katika nchi kwa sababu taarifa nyingi tunaripoti sisi na watu wanazisikia na kuamini hivyo ni sehemu muhimu na tufanya fanya kazi kubwa hivyo tusichoke kupiga kelele kuhusu ndoa za utotoni na mabadiliko ya sheria,”anasisitiza James.

TAMWA KUJIVUNIA WAANDISHI

Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari wanawake Tanzania  (TAMWA), Dk Rose Reuben anasema juhudi zinazofanywa na waandishi wa habari katika kukabiliana na ndoa za utotoni ni kubwa kwani matukio yanaripotiwa mfululizo na pia elimu inatolewa.

“Sisi kama TAMWA tunaona sio haki mtoto kuolewa, tunataka waingie kwenye ndoa wakiwa watu wazima tunakataa kuona mtoto anaingia katika mkataba ambao sio kwa hiari yake,  hivyo tunatamani kuona waandishi kuendelea kuandika na kutangaza kuhusu mabadiliko ya sheria,”anasisitiza Dk Rose.

Anasema madhara ya mtoto  kuolewa yamethibitishwa kiafya na hata akienda hospitali ataenda kwa madaktari, hivyo anapewa majukumu makubwa ya kuwa mke na mzazi wakati bado hajawa na uelewa wowote.

“Lakini pia inakuwa ngumu kujiunganisha na mambo mengine kama biashara na kufanya kazi kwani sheria imeondoa haki yake ya kujihusisha na mambo mengi na sheria inamtambua mtu mzima akiwa na miaka 18,”anasema.

ASASI KUTOA ELIMU

MEDEA-Tanzania ni taasisi inayotumia vyombo vya habari na kazi sanaa katika kuibua changamoto zinazowakumba mabinti, wanawake na vijana katika jamii.

Suala la ndoa za utotoni lipo ndani ya ajenda kwani ni kikwazo muhimu kwa wasichana kufikia ndoto zao.

Ofisa Habari wa MEDEA, Jackline Mgeni anasema  wanafanya kazi ya kuongeza uelewa wa jamii kuhusu sheria ya ndoa ya Tanzania, ambayo inaonekana kuchochea changamoto hii ya ndoa za utotoni, na kutetea marekebisho yake.

“Tunahimiza ushiriki mkubwa wa jamii katika vuguvugu hilo katika kuchochea na kuharakisha juhudi za wabunge za kurekebisha sheria, ambayo tayari iliamuliwa kuwa ni kinyume cha katiba na Mahakama Kuu mwaka wa 2016, katika kesi ya kimkakati ya Rebeca Gyumi dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Pamoja na hayo anasema wamekuwa na miradi kama Sauti Zetu ambapo ulifanya katika mikoa minne ya Tabora, Kigoma, Lindi na Mtwara ambapo shughuli kubwa katika mradi huu ilikuwa ni kuongeza uelewa kwa wananchi juu ya masuala ya ndoa za utotoni na kuifanya jamii iwe na sauti moja ikipinga uwepo wa sheria ya ndoa ya mwaka 1977.

Anasema wamekuwa wakitumia filamu ambayo imekuwa ikielezea masuala ya ndoa za utotoni na wakifanya midahalo mbalimbali na wananchi ambao wanaeleza mitizamo yao juu ya masuala ya ndoa za utotoni kwenye jamii zao na njia wanazoweza tumia ili kupambana na changamoto hii katika jamii yao.

“Pia tunafanya dodoso kupima uelewa wa watu juu ya ndoa za utotoni na kama wanafahamu uwepo wa sheria hii,” anasema.

Anaeleza kuwa mradi mwingine ni  Ajenda Yetu ambao umefanyika Kishapu-Shinyanga, ambao lengo lake lilikuwa kuwaweka wananchi na vyombo vya habari katikati ya kiini cha mapambano dhidi ya ndoa za utotoni.

“ Kupitia midahalo ya wazi ya jamii na redio za jamii, uelewa wa wananchi juu ya madhara ya ndoa za utotoni ilifanyika, na wakapewa nafasi ya kuzungumza na viongozi wao wa mitaa kuhusu jinsi wanavyoweza kushawishi marekebisho ya sheria ya ndoa,” anasema.

SERIKALI YAJIPANGA

Waziri wa Sheria na Katiba,Dk  Damas  Ndumbaro anasema wadau wengi wanaongea sheria ya ndoa na mahakama ya rufani ilitoa maelekezo kwamba umri wa mtoto kuoa na kuolewa lazima ubadilishwe na usiwe chini ya miaka 18.

Anasema maamuzi ya Mahakama ya Rufani ni mahakama ya juu zaidi Tanzania ambayo ukitaka kupinga maamuzi yale lazima uombe marejeo, ambayo watakaa majaji saba na mpaka sasa kama serikali haijafanya hivyo na wala hamna aliyepinga maamuzi hayo .

Baadhi ya wananchi wa Kishapu wakiwa kwenye mdahalo wa wazi na viongozi wao wakijadili namna gani wanaweza kuchochea mabadiliko ya sheria ya ndoa ya mwaka 1977, ambayo imekuwa ikichangia kukithiri kwa ndoa za utotoni kwenye jamii hasa za wafugaji.

“Serikali tulichukua na kupeleka bungeni lakini Bunge kwa busara yake ilitukumbusha kuwa sheria hii wakati inatungwa 1970 ilitanguliwa na whitepaper ambayo ilijumuisha maoni ya wadau wote ,”anasema na kuongeza:

“Ndio maana ikafanya sheria ya ndoa iwe ya kipekee duniani ambapo ndoa nne zinapatikana chini ya sheria moja kuna ndoa za kiislamu,kikiristo, kimila na ndo za serikali zipo sasa bunge ilituelekeza tufanye mawasiliano tupate maoni na twende na mapendekezo na katika maoni hayo tumejifunza mengi.

Dk Ndumbaro anasema jambo  ambalo  wamejifunza ni kwamba wakati wanatunga sheria hiyo serikali ilipende kuwa umri usiwe chini ya miaka 16, wakati ule wa miaka ya 70, lakini Umoja wa Mataifa ulishauri angala mpaka 14.

“Hivyo miaka 14 haikutokana na dini yoyote ilitokana na ushuri wa kimaadishi kutoka Umoja wa Mataifa sasa leo Umoja wa Mataifa kupitia UN-WOMEN na UNICEF wanashauri angalau miaka 18 kama mahakama ilivyopendekeza,”anafafanua.

Aidha anaeleza kuwa baada ya kupata ushauri kama wizara wamekamisha maoni  na mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ambao unasema umri wa kuoa na kuolewa sio chini ya miaka 18.

“Hiyo ni moja ya kutekeleza maagizo ya mahakama na utawala wa sheria unataka hivyo, amri za mahakama lazima zitekelezwa isipokuwa imepingwa kwa rufaa au marejeo. “

Anaongeza: “Lakini pili katiba yetu ya ambayo tunayo inamtambua mtoto ni mtu mwenye umri chini ya miaka 18 ,sheria ya mtoto inamtambua kama mtu mwenye umri wa miaka 18 na sheria hizi sasa zimesema mtoto kuna haki ambazo hatakiwi kuzipata mfano mtoto hawezi kuajiriwa ,hawezi kupewa leseni ya udereva, hawezi kupiga kura, kushiriki kwenye shughuli za kisiasa lakini pia hana uwezo wa kuingia mikataba,” anaainisha Dk Ndumbaro.

Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Damas Ndumbaro.

Anahoji kuwa kama mtoto amezuiwa kufanya mambo hayo inakuwaje aruhusiwa aoe au kuolewa?

“Kwa hiyo ndo kusema kuoa ni jambo dogo kuliko kupata leseni ya udereva? Au kuolewa ni jambo dogo kuliko kupata leseni ya udereva? Hapa unaona kama tumekubali kwa mujibu wa katiba na sheria kuwa mtoto ananyimwa haki fulani kwa sababu ya umri wake lazima tulitekeleze hili,”anasisitiza.

Anawaomba wadau kuunga  mkono maelekezo ya muhimili wa mahakama, ambapo serikali sasa itakwenda kuwasilisha bungeni na watoe maoni kwa uwazi na uhuru ili yatumike kujenga nchi yenye maadili,ambayo inaheshimu imani za kidini na mila na desturi.

Muswada wa sheria hiyo unatarajiwa kuwasilishwa bungeni baada ya mchakato wa kukusanya maoni kukamilika.