Waandishi wa habari wafundwa
SONGWE: WAANDISHI wa habari nchini wametakiwa kuwa mabalozi kulisaidia Jeshi la polisi kuibua matukio mbalimbali ya kihalifu yakiwemo madhila yanayowakuta wakiwa katika majukumu ya kutafuta habari ili kuhakikisha Jamii inakuwa salama pamoja mali zao.
Hayo yamesisitizwa na Kamishina Msaidizi wa Polisi Gallus Hyera akimwakilisha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe katika mdahalo na waandishi wa habari na Jeshi la polisi ,alisema waandishi wa habari ni watu muhimu sana kwa sababu hufanya kazi nyingi ambazo husaidia jeshi hilo kupata taarifa mbalimbali za uhalifu.
Alisema Pamoja na ushirikiano mzuri wa Jeshi la polisi na waandishi wa habari Mkoa wa Songwe umekuwa na changamoto kwa baadhi ya askari wachache kutofuata maadili na Sheria zinazowaongoza hivyo kuwasababishia madhila wandishi wa habari.
“Mnapopata changamoto za aina zozote zinazoathiri utendaji wenu toeni taarifa mara moja tutawapa ushirikiano wa kutosha tutawachukulia hatua”.
“Hivyo Hivyo Kuna baadhi ya waandishi wachache kama ilivyo kwa maaskari wanakiuka misingi yenu ya maadili , tukemee ukanjanja kwenye hizi Kazi zetu ” amesema Kamishina Hyera.